Imeandikwa na Isdory Kitunda
SHIRIKA la Maendeleo ya Kijamii nchini (TSSF) limesema kuwa linafanya
kazi zake kihalali na kuwa kesho asubuhi litawasilisha nakala za
uhalali wake huo kwenye Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mwishoni mwa wiki, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako katika Mkutano wa Bunge unaoendelea
Dodoma, akimjibu Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi aliyeomba
mwongozo kuhusu uhakika wa TSSF katika kutoa mikopo nafuu kwa wanafunzi
wa elimu ya juu, alikana kulifahamu na kutaka watu kulipuuza.
Kutokana na kauli hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TSSF, Donati Salla, jana
alitoa taarifa akisema kesho ataenda wizarani kujielezea kuhusu
uendeshwaji wa shughuli zake hizo akiwa na nakala muhimu za shirika
hilo.
Salla alisema hadi jana hakuwa amepewa barua rasmi ya kumtaka
kuripoti, lakini hata hivyo alisema kwa sasa shirika lake halina
mrejesho wa kusema dhidi ya tamko la Waziri Ndalichako kuhusu yeye na
wizara yake kutoitambua TSSF licha ya shirika hilo kufanya jitihada
mbalimbali za kujitambulisha kwa wizara.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment