Imeandikwa na Mwandishi Wetu
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza
orodha nyingine ya wanafunzi 1,775 wa mwaka wa kwanza huku ikifungua
dirisha la rufaa hadi Novemba 19, mwaka huu.
Kutolewa kwa orodha ya wanafunzi 1,775 waliopata mikopo, kunafanya
jumla ya wanafunzi 31,353 waliopewa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa
kwanza pekee. Katika awamu ya kwanza, Bodi ilitangaza majina ya
wanafunzi 10,196, awamu ya pili wanafunzi 11,481 na awamu ya tatu
wanufaika 7,901. Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi Mtendaji wa HELSB, Abdul-razaq Badru (pichani) katika taarifa
yake kwa vyombo vya habari.
Badru alisema orodha na majina iliyotolewa tayari imeshatumwa kwa
vyuo husika ili kuwawezesha wanafunzi kufanya usajili na kuendelea na
masomo. “Tumekuwa tukifanyia kazi orodha za udahili ambazo tumekuwa
tukipokea, na kila tunapokamilisha, tunatoa orodha za wanafunzi
waliopangiwa mikopo ambao wana sifa, leo (jana) tumetoa majina ya
wanafunzi 1,775,” alisema Badru.
Serikali imetenga Sh bilioni 427.54 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi
kwa mwaka 2017/2018 na tayari Serikali imeshatoa Sh bilioni 147.06 kwa
ajili ya robo ya kwanza ya mwaka huu. Katika fedha hizo, Sh bilioni
427.54, ni kwa ajili ya wanafunzi 122,623 wa mwaka wa kwanza na
wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo.
Akizungumzia kufunguliwa kwa dirisha la rufaa, Badru alisema bodi
imefungua dirisha la rufaa kuanzia leo hadi Novemba 19, mwaka huu ili
kuwapa fursa waombaji wote ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo
kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili.
“Lengo la HESLB ni kuhakikisha wanatangaza orodha ya majina ya
waombaji mikopo waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo au kabla ya
Novemba 30, mwaka huu. “Tunatoa mwito kwa uongozi wa vyuo vyote kupokea
maombi ya rufaa za wanafunzi na kuwasilisha kwa bodi ya mikopo kabla ya
Novemba 22 mwaka huu ili kuiwezesha bodi kutoa orodha ya waombaji
waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo Novemba 30,” alieleza.
Hivi karibuni, HELSB ilisema wanafunzi ambao hawakupangiwa mkopo ni
pamoja na waliokuwa na udahili chuo kikuu zaidi ya kimoja na
waliothibitisha awali wakitaja chuo watakachokwenda lakini baadaye
wakabadilisha.
Kundi lingine la waliokosa mikopo ni pamoja na waliowasilisha maombi
yakiwa na dosari kadha wa kadhaa na wengine wakiwa na sifa pungufu za
uhitaji wa mkopo. Kutokana na malalamiko ya wanafunzi waliokosa mikopo,
bodi iliahidi kufungua dirisha la rufaa ya kupata mikopo ili kuwapa
fursa wanafunzi ambao hawajaridhika kuwasilisha rufaa zao kupitia vyuo
walivyopata udahili na majina ya watakaofanikiwa kupata mikopo
yatatolewa.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment