Imeandikwa na Maulid Ahmed, Dodoma
SERIKALI imeviagiza vyuo vyote vya elimu ya juu kusajili wanafunzi,
kuwapatia fedha zao za mikopo na watakaowasumbua watafungiwa.
Aidha imesema mpaka sasa wanafunzi 29,578 wa mwaka wa kwanza
wameshapelekewa fedha zao za mikopo walikodahiliwa. Hayo yalibainishwa
jana bungeni na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako wakati akitoa kauli ya serikali kuhusu
udahili na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu mwaka
2017/2018.
Kauli hiyo ilitokana na Bunge kuiagiza serikali kutoa kauli kuhusu
udahili na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi hao kutokana na mwongozo wa
Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM).
“Serikali haitasita kuchukua hatua kali ikiwemo kuvifungia vyuo
vitakavyoleta usumbufu usio wa lazima kwa wanafunzi na kuwafanya
wapoteze muda ambao wanapaswa wautumie kwa masomo, UDOM (Chuo Kikuu cha
Dodoma) na Chuo cha Mwalimu Nyerere wana urasimu kupokea wanafunzi, Chuo
Kikuu Mwenge nimeona kinawalazimisha wanafunzi kubadilisha kozi na
wanawaambia kozi zimejaa wakati waliomba na wakapata...tutavifungia vyuo
vyote vinavyosumbua wanafunzi na kuwafanya wawe wazururaji mitaani,”
alisema.
Profesa Ndalichako ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na
Kurugenzi ya Elimu ya Juu ya Wizara ya Elimu kufuatilia kwa karibu mambo
yanayoendelea vyuoni wakati wanafunzi wanaripoti na kuwabainisha wote
wanaokiuka taratibu na kuwanyima wanafunzi haki yao ya kusoma programu
wanazotaka.
Alisema kwa wanafunzi walioripoti vyuo tofauti na mikopo yao
iliyopelekwa vyuo vingine, mikopo yao itahamishiwa kwenye vyuo
walivyodahiliwa baada ya kupokea uthibitisho kutoka katika vyuo
vilivyowapokea.
Alisema hadi Novemba 07 wanafunzi 29,578 wa mwaka kwanza walikuwa
wamepangiwa mikopo kati ya wanafunzi 30,000 wanaostahili. Alisema
serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Ellimu ya Juu imepanga kutumia Sh
bilioni 427.54 kugharamia mikopo kwa wanafunzi 122,623 ambapo 30,000 ni
wa mwaka wa kwanza na 92,623 ni wanaoendelea na masomo.
Katika robo ya kwanza ya mwaka huu, Wizara ya Elimu imepokea Sh
bilioni 147.06 kwa ajili ya ada za wanafunzi hao kugharamia chakula,
malazi, vitabu, viandikia na mahitaji ya masomo.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment