SERIKALI imeviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kulichunguza Shirika
la Tanzania Social Support Foundation (TSSF) kutokana na kudaiwa
kuwahadaa Watanzania linatoa mikopo na wanafunzi 198 wakarubuniwa kwamba
watapewa mikopo ya zaidi ya Sh milioni 533.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi,
William Ole Nasha pia amepiga marufuku shirika hilo kujihusisha na
utoaji mikopo na amezifunga akaunti zake zote baada ya kujiridhisha
hakuna hata chembe ya shirika hilo kuwa na uwezo wa kutoa mikopo.
“Naviagiza vyombo vya usalama kuwakamata na kuwahoji viongozi wa
shirika hili, kuwauliza ukweli kuhusu huduma za utoaji mikopo na
kujiridhisha kuhusu mkakati wa kuwaibia na sheria ichukue mkondo wake,”
alisema Waziri.
Alisema shirika hilo ni la kitapeli kutokana na kuwatoza wanafunzi Sh
30,000 kila mmoja za kujisajili wakati haina fedha kwenye akaunti.
Alisema viongozi wa shirika hilo wamesema walitegemea kupata fedha
kutoka Kampuni ya Cagney la Marekani ambapo kwanza walitakiwa kutoa dola
50,000 ili wawape ufadhili huo.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Donati Salla alikiri kuwatoza wanafunzi
Sh 30,000 na akaahidi kuzirudisha mapema Serikali itakavyoagiza na wapo
tayari kuendelea kutoa usajili bure kwa wanafunzi kwa lengo la
kuwasaidia Watanzania.
Ofisa Utawala, Marwa Charles alisema shirika lao si la kiserikali,
hivyo si lazima liwe na fedha linapotoa huduma na si lazima lioneshe
kiwango cha fedha kilicho benki bali linatoa huduma tu.
Charles alisema kulikuwa na matatizo katika shirika hivyo wakachelewa
kutuma dola 50,000 za Marekani sawa na Sh milioni 112 Novemba 12, mwaka
huu nchini Marekani ili wapate fedha za kukopesha wanafunzi 50,000.
Waziri Ole Nasha alisema shirika hilo ni la kitapeli kwa sababu
limetumia fursa ya uhitaji wa mikopo kwa wanafunzi kudanganya ambapo
wanafunzi 600 waliomba mikopo wakati likijua halina fedha zaidi ya Sh
milioni 60 au 70 tu.
“Shirika hilo ni la kitapeli”, Ole Nasha alisema na kuongeza katika
mkataba na Kampuni ya The Cagney ya Marekani, hakuna mahali popote
palipoonesha itatoa fedha kuwafadhili wanafunzi, badala yake viongozi
walikuwa wakiulizia uwezekano wa kufanya harambee.
Waziri ole Nasha alisema katika mkutano na viongozi wa taasisi hiyo,
alisema wamebaini TSSF haina uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi 50,000,
bali ulikuwa utapeli wa kupata Sh 30,000 za ada za kujiandikisha.
Alisema hakuna sehemu ya kupata fedha na serikali inatoa taarifa kwa
umma ufahamu shirika hilo halina uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi
waliokwishaanza masomo vyuoni wakitegemea kupata mikopo Desemba 20,
2017.
Japo taasisi hiyo ilisajiliwa kihalali nchini, serikali imebaini
kwamba bajeti yake kwa mwaka ni Sh milioni 2.5, hivyo kusingekuwa na
miujiza kuwa na uwezo wa kuwa na fedha za kutosha kufadhili wanafunzi
50,000 kwani historia haioneshi uwezo huo wa kifedha.
Alisema shirika hilo lilikuwa na nia mbaya ya kuwahadaa wanafunzi na
lilidai wangekosa fedha Marekani, wangepata China ambako pia hakuna
mkataba wa makubaliano ya fedha.
Wanafunzi 198 walioahidiwa mikopo na shirika hilo walikuwa wameomba
kusoma vyuo vikuu vya Dar es Salaam (UDSM), Nyegezi (SAUT), Chuo Kikuu
cha Tiba Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA),
Morogoro na vingine walitozwa Sh 30,000 za kusajiliwa jumla yake ikiwa
Sh milioni 5.94.
Kutokana na uhaba wa mikopo ya wanafunzi katika Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu (HESLB), zaidi ya wanafunzi 600 walikuwa wameahidiwa
watapewa mikopo na shirika hilo na kurudisha fedha kwa riba ya asilimia
sita.
Naibu Waziri ole Nasha alisema, serikali itaangalia namna ya
kuwasaidia wanafunzi hao waliotapeliwa na shirika hilo kwani wanaweza
kushindwa kuendelea na masomo yao kwa sasa.
Mkutano na waandishi wa habari ulipomalizika, viongozi wa shirika
hilo, Salla na Charles walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa Polisi
kwenda kutoa maelezo kuhusu nia hiyo ya kutapeli wanafunzi wenye shida
ya mikopo.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment