Na. Thobias Robert - MAELEZO
Tume
ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) itaendelea kusimamia kwa umakini ubora wa
elimu vyuo vikuu ili kuzalisha wasomi wenye tija kwa Taifa na kuongeza
ufanisi, ubunifu, maadili pamoja na utendaji kazi uliotukuka kwa vijana
wanaohitimu elimu ya vyuo vikuu nchini.
Hayo
yamesema leo na Afisa Habari Mwandamizi wa TCU Edward Mkaku wakati wa
mahojiano na mwandishi wa habari hii katika maonesho ya vyuo vikuu
yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini, Dar es Salaam.
“Kwa
sasa TCU tunaratibu udahili ambao unafanywa na vyuo vikuu vyenyewe,
wakishamaliza kudahili majina yataletwa kwetu, na sisi tutapitia majina
yote ili kuyahakiki kama yana vigezo vyote vya kujiunga na chuo husika.
Tutashirikiana na Baraza la Mitihani na tukigundua kuna mtu amechomekewa
kujiunga na chuo akiwa hana vigezo tutamuondoa,” amefafanua Mkaku.
Amesema
kuwa tume hiyo itatembelea vyuo vyote nchini ili kufanya ukaguzi wa
jina kwa jina kwa ajili ya kujiridhisha, na kama ikitokea hakuna kasoro
yoyote basi mwanafunzi ataendelea na masomo.
Mkaku
aliongeza kuwa, ingawa zoezi la udahili limerudishwa vyuoni lakini bado
TCU ina mamlaka ya kusimamia ubora, mwenendo, mitaala pamoja na kozi
zinazotolewa vyuoni ili kukuza na kuendeleza elimu bora kwa ajili ya
kuinua Taifa hasa wakati huu ambapo Taifa linaelekea katika mapinduzi ya
uchumi wa viwanda.
Aidha
amewataka wahitimu wawe makini katika kuzisoma kozi na kuchagua ili
kusiwepo na mkanganyiko na malalamiko yanayotokana na kukosea kuchagua
au kupangiwa kozi ambayo mhitimu hakuomba.
Hapo
nyuma zoezi la udahili wa vyuo vikuu lilikuwa likifanywa na TCU, lakini
kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi ya wanafunzi ya kupangiwa vyuo
au kozi ambazo hawakuzichagua ama kuzipenda, mapema mwaka huu Rais Dkt.
John Pombe Magufuli alisitisha zoezi la udahili kupitia TCU na kuagiza udahili kufanyika moja kwa moja vyuoni kuanzia mwaka wa masomo wa 2017/18.
No comments:
Post a Comment