Imeandikwa na Waandishi Wetu
BAADHI ya vyuo vilivyosimamishwa kufanya udahili katika baadhi ya
programu zake, vimebainisha kuwa vimeanza kuchukua hatua ya kuondoa
dosari hizo, na viko tayari kufanyiwa uhakiki tena.
Hayo yamebainishwa jana kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam
kwenye maonesho ya 12 ya Taasisi za Elimu ya Juu nchini yanayoendelea
katika viwanja vya Mnazi Mmoja. Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha
Mtakatifu Augustine (SAUT), Padri, Thadeus Mkamwa alikiri kuwa baadhi
ya matawi ya chuo chake, yamesimamishiwa udahili katika baadhi ya
programu zake, lakini ni kutokana na tatizo la mawasiliano baina ya chuo
hicho na TCU.
“Ni kweli walituletea notisi ya siku 14 tujibu kuhusu upungufu
waliobaini, tumewajibu mapema tu, lakini wakati tunasubiria matokeo,
tukasikia kwenye vyombo vya habari kuwa, baadhi ya programu zetu
zimesimamishwa zisifanyiwe udahili, lakini tunalifanyia kazi,” alisema
Mkamwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Vyuo Vikuu vya Kanisa Katoliki,
Atunus Simwambi, alikiri kuwa programu iliyosimamishiwa udahili ilikuwa
kwa muda wa miaka mitatu angu ianzishwe haijawahi kuwa na wanafunzi na
hivyo kutofundishwa chuoni hapo.
“Programu hii ilianzishwa kwa ajili ya watu wanaotakiwa kuwa mapadri
au wanaokwenda kufanya kazi za utume katika maeneo mbalimbali. Kwa kuwa
kuna mchakato wa kuunganisha chuo chetu na Chuo cha Filosofia cha
Kibosho, tulitarajia programu hii itarejea,” alisema. Chuo hicho
kimesitishiwa programu moja ya Bachelor of Arts in Philosophy with
Ethics. Naye Makamu wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro (MUM), Profesa
Hamza Njozi, pamoja na kukiri kuwa katika baadhi ya programu
zilizosimamishwa udahili zilikuwa na changamoto ya walimu, alieleza kuwa
dosari hizo zimefanyiwa kazi kama ambavyo Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
(TCU) ilivyoagiza katika notisi yake ya siku 14.
Alisema chuo hicho kilipatiwa notisi ya siku hizo 14 inayoanzia Julai
Mosi hadi 14, mwaka huu, kufanyia marekebisho dosari hizo, lakini hata
baada ya kutoa majibu, walishtukia kupitia vyombo vya habari, kuwa
programu hizo zimesimamishiwa udahili. Akizungumzia taarifa ya TCU,
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Watoa Elimu Wasiotegemea Serikali
Kusini mwa Jangwa la Sahara(CIEPSSA), Benjamin Nkonya alisema uamuzi huo
wa serikali ni nzuri kwani una nia njema ya kurudisha heshima ya elimu
nchini.
Nkonya alisema hatua hiyo inapaswa kuungwa mkono na wadau wa elimu
nchini kwa sababu yapo baadhi ya mambo ambayo yamechangia kiwango cha
elimu kushuka wakiwemo baadhi ya wasomi ambao wameonesha udhaifu kwenye
utendaji wao. “Kwanza kabisa tunaona jinsi rais anavyokerwa na baadhi ya
wasomi ambao wanavuruga nchi badala ya kuwa kioo, ameona hakuna
mwelekeo nah ii inawezekana ikatokana na mfumo wa elimu ambao wakati
mwingine baadhi ya shule au vyuo vimetoa elimu isiyokidhi, sasa
tunapojisahihisha ni vizuri ili tuwe na mfumo thabiti kwa manufaa ya
taifa,” alisema Nkonya.
Alisema kwa bahati nzuri sekta ya elimu nchini kwa sasa imepata mtu
sahihi kwenye wizara hiyo inayoongozwa na Profesa Joyce Ndalichako
ambaye hata wao wana imani ataendelea kuiboresha zaidi kwa sababu
utendaji kazi wake unatambulika. “Profesa Ndalichako ni mtu makini,
nakumbuka nilipokuwa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo
Visivyo Vya Serikali (TAMANGSCO) zaidi ya miaka 10, Profesa Ndalichako
alipokuwa NECTA, aliadhibu shule au vyuo vilivyokosea, na alitoa adhabu
kali hata wakati mwingine kufutia matokeo shule nzima alipobaini
udanganyifu, alifanya hivyo kulinda heshima ya elimu,” alisema Nkonya.
Hivyo akashauri kuwa uamuzi uliofikiwa na serikali kupitia TCU ni uamuzi
sahihi na kuvishauri vyuo husika kufuata maelekezo ili kuhakikisha
kiwango cha elimu kitolewacho kina ubora unaotakiwa.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment