Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, ameiagiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu
nchini (NBAA) kuwachukulia hatua wale wote wanaoitia doa taaluma hiyo kwa
kufanya ubadhilifu wa fedha za umma.
Maagizo
hayo yametolewa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango,
wakati wa Uzinduzi wa Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC) uliokwenda sambamba na
ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa wahasibu unaojumuisha wadau kutoka nchi za Afrika
Mashariki, katika eneo la Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Amesema
kuwa Idadi ya Wahasibu wenye sifa inazidi kuongezeka na hivyo kuisaidia Serikali,
japo kuwa Serikali hairidhiki kuona wanataaluma wa Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu
(CPA) wanaongezeka huku vitendo vya ubadhilifu wa fedha za Umma na ufisadi vikiendelea
kuripotiwa.
“Wapo
hata wahasibu wanaotumia taaluma yao vibaya, wanaowawezesha wafanyabiashara
kukwepa kodi, wanachakachua vitabu vya taarifa za fedha na kufanya ufisadi kwa
njia ya kalamu na kompyuta jambo ambalo halikubaliki hata kidogo” Aliongeza
Dkt. Mpango
Amesema
kuwa machozi ya masikini wa Tanzania yatawafuata mafisadi hadi kaburini lakini
serikali ya Awamu ya Tano haitasubiri hao mafisadi wafe, itawatumbua na wala
hakuna mzaha na kwamba tayari mahakama ya mafisadi imeanza kazi na
itawashughulikia.
Aidha,
Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewaasa wanataaluma wa
uhasibu na ukaguzi wa hesabu kuitumia taaluma yao kuisaidia Serikali katika
hatua yake ya kuelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda kwa kuwa
taaluma hiyo ina umuhimu mkubwa.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu,
Bw. Pius Maneno amesema kuwa, Kituo hicho kilichozinduliwa cha APC hadi
kumalizika, kitagharimu Sh. Bilioni 35 ambapo mpaka sasa fedha zilizotumika ni
takribani Sh. Bilioni 31.5.
“Gharama
halisi za ujenzi wa kituo hicho zilikuwa Bilioni 14 lakini kutokana na mzabuni
wa ujenzi kuchelewesha ujenzi ndio maana kumekuwa na Ongezeko la kiasi hicho
cha fedha” aliongeza Bw. Maneno.
Ujenzi
wa kituo hicho ambao uko katika eneo lenye ukubwa wa takribani ekari 14
umehusisha ujenzi wa Kumbi za mikutano zinazochukua zaidi ya watu 1600, viwanja
vya michezo na vyumba vya kisasa 108 vya kulala wageni.
Bw.
Maneno amesema kuwa kujengwa kwa kituo hicho kutaifanya Bodi hiyo kuokoa kiasi
kikubwa cha fedha kilichokuwa kikitumika kukodi kumbi za kufanyia na kusahisha
mitihani ya Bodi (NBAA).
Amezitaja
faida zingine kuwa ni kuboreshwa kwa mazingira ya kitaaluma na wanataaluma wa uhasibu
pamoja na kuimarika kwa utawala bora na
kuwa chachu ya uchumi wa viwanda, kwa kuwa Kituo hicho, kinatoa elimu bora
itakayowawezesha wahitimu kuingia kwenye ushindani ndani ya nchi za Afrika
Mashariki na Duniani kwa ujumla.
Ujenzi
wa Kituo hicho umedhaminiwa na serikali kupitia mkopo kutoka Mfuko wa Hifadhi
ya Jamii-NSSF, Bodi ya Uhasibu-NBAA na Mbia mwenza wa kituo hicho, Mfuko wa Pensheni
ya Watumishi wa Serikali-GEPF.
Mwisho
No comments:
Post a Comment