Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. insta : @matukionawanavyuo Tumieni mtandao huu ni wenu nyote.
WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imetoa
ufafanuzi kwamba haijapiga marufuku watu wenye Stashahada wenye sifa
kujiunga na vyuo vikuu badala yake walichokataza ni wanafunzi waliofeli
kidato cha nne na cha sita kujiunga na vyuo vikuu bila kuwa na vyeti
vyenye sifa.
Aidha, imesema kwa waliomaliza kupitia mfumo huo na wapo kazini ni
wajibu wa waajiri wao kuhakikisha wana sifa za kazi wanazofanya na
kutumia fursa hiyo kufanya mitihani ili kuwa na sifa zinazohitajika.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Stella Manyanya alitoa ufafanuzi huo
jana Dar es Salaam kutokana na taarifa za upotoshaji zilizoenea
mitandaoni kwamba serikali imepiga marufuku watu wenye Stashahada
kujiunga na vyuo vikuu badala yake watakaoingia ni wenye sifa za kidato
cha sita.
Manyanya alisema kwa waliopo vyuoni kwa sasa wanatakiwa kuhakikisha
wanakuwa na sifa za shahada kwa kusafisha vyeti vyao na wapewe fursa ya
kufanya mitihani hiyo waliyofeli na kama wamefaulu kozi hiyo, pia
wataweza kufaulu mitihani hiyo itakayowapa sifa ya kusoma vyuo vikuu.
“Ni vitu tunavyovifanya wenyewe ila vina madhara makubwa, unakuta mtu
anakaa nafasi kwa sababu ana vyeti, lakini uwezo hana… uhakiki
utafanyika kwa vyeti na wanaofanya hivyo ni Utumishi,” alisema Naibu
Waziri.
Alisema kwa watakaobainika pia kuingia vyuoni kwa sifa ambazo
zilikuwa hazitakiwi kwa wakati huo ni batili zitafutwa na kwa
watakaoingia kwa sasa vyuoni kwa kutumia njia zisizo rasmi na kubainika
hata ikifika mwaka 2020 watafutwa kwa kuwa taarifa tayari wanayo.
“Kilichoongelewa siku ile ni kuruhusu kidato cha nne na kidato cha
sita waliofeli kuingia kwenye ‘foundation course’ na diploma haikutajwa
pale kwa kuwa haikuulizwa na hakuna kauli iliyotajwa pale kukataza watu
wa diploma kwenda chuo kikuu,” alieleza Manyanya akirejea kauli ya
Waziri wake, Profesa Joyce Ndalichako hivi karibuni katika mahafali ya
Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) yaliyofanyika mkoani Pwani.
Profesa Ndalichako alikaririwa akisema vigezo vya udahili vinatakiwa kuzingatiwa.
“Nami ningependa nizungumzie kwamba foundation course hazimuongezei
mtu sifa. Kama sifa ya kujiunga na chuo kikuu ni kufaulu kidato cha
sita, kama amefeli Baraza la Mitihani linaruhusu kurudia mtihani, kwa
nini anakwepa kule? Kwa nini? Kwa nini tunataka tuendeleze uchochoro,”
alieleza Waziri Ndalichako.
Naibu Waziri alisema kuna njia mbili za kwenda chuo kikuu ikiwemo
njia ya moja kwa moja na njia ya mbadala ya kuwa na vyeti
vinavyotambulika na kinasimamiwa na mamlaka husika ambayo ni Baraza la
Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na wawe na ufaulu mzuri.
“Tanzania imejiwekea mifumo yake ya elimu ambayo inaendana na ngazi
za kimataifa katika utoaji wa elimu na hapo awali tulikusudia
kuhakikisha elimu inatolewa kwa watu wengi zaidi na hizo fursa
zinawafikia wadau wote katika ngazi mbalimbali kwa kupanua elimu ya
msingi hadi vyuo vikuu,” alieleza Naibu Waziri.
Alisema walitambua kuna wadau mbalimbali walitamani kusoma vyuo
vikuu, lakini hawapati hiyo fursa na ndiyo wakaanzisha mfumo huo wa Chuo
Kikuu Huria na mtu anaweza kusoma alipo na mfumo umekuwa ukiboreshwa
siku hadi siku.
Alisema iliwekwa mifumo ya vyeti na ngazi zake kulingana na vigezo na
hivyo siyo kila cheti kinachotolewa kinaruhusu mtu kwenda ngazi
nyingine na kila mamlaka imepewa jukumu ili kulinda ubora wa elimu
unaotolewa nchini.
Naibu Waziri alisema kutokana na uanzishwaji wa vyuo mbalimbali
kumejitokeza changamoto na watu kutoka katika mfumo rasmi uliopangwa na
kujiwekea mifumo binafsi ambayo imeingiza hata wanafunzi wa kidato cha
nne ambao hawana sifa kuingia vyuo vikuu.
“Jambo hilo limesababisha kuwepo kwa msuguano, haiwezekani mtu afeli
kidato cha nne bila kuwa na cheti kingine chochote anaingizwa katika
kozi hiyo halafu anaingizwa chuo kikuu, sisi hatujarasimisha mfumo huo
wa ‘foundation course’ na hatuna vipimo vyake,” alieleza.
Alisema kwa kawaida mwanafunzi mwenye diploma inayotambulika
wamewekewa usawa wa alama fulani na kidato cha sita hivyo wanakuwa na
sifa ya kuingia vyuo, lakini siyo waliofeli hivyo wanatakiwa kufanya
utafiti zaidi katika kozi hiyo.
“Haiwezekani kila mtu akajianzishia mfumo wake tu, tulifikia eneo
ambalo si zuri kama nchi na sasa tutaimarisha ubora…ukifeli kidato cha
nne unatakiwa kwenda kusoma na kupata cheti kwenye mtaala unaotambulika
na ukaenda diploma na unapofaulu unaweza kwenda chuo kikuu,” aliongeza.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila alisema
suala la ‘Foundation course’ limelenga kumuandaa mtu mwenye sifa ambaye
amekuwa nje ya mfumo kwa muda mrefu ili kuingia chuo kikuu, lakini
walichokuwa wakikifanya wengi ni kuwachukua waliofeli kidato cha nne na
sita na kuwaingiza katika kozi hiyo na hatimaye kuwaingiza chuo kikuu.
Awali, baadhi ya wadau wa elimu nchini waliozungumza na gazeti hili
wakiwemo wanataaluma walisema wanasubiri kupata taarifa rasmi kutoka
wizarani kuhusu madai hayo, lakini wakaeleza manufaa ama athari za
kutumika kwa mfumo huo nchini.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dares Salaam, Dk Benson Bana alisema
haamini iliyonukuliwa ilikuwa kauli rasmi ya serikali, lakini akaongeza,
“Upo utaratibu mbalimbali wa kuingia vyuoni na walio wengi wamepitia
mfumo wa kuanzia cheti na kujiendeleza hadi kufika chuo kikuu na
kutunukiwa digrii wakiwemo maprofesa na madaktari wengi.”
Alisema mfumo huo unasaidia kupata wanafunzi wengi wenye uzoefu na
ambao huwasaidia wenzao katika kufanikisha elimu yao na huo ndio mfumo
unaotakiwa.
Dk Bana alisema jambo linalotakiwa kutazamwa ni uwepo wa vyuo vingi
vikuu ambavyo vimekuwa vikigawa alama za ajabu kwa wanafunzi, lakini
wanapoingia vyuo mtihani ndio utakaowapembua.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch
alisema “Elimu ya kujiendeleza kuanzia ngazi ya cheti na kuendelea
diploma, digrii na hata kufikia uzamivu ni mfumo uliopo dunia nzima.”
Alisema wapo wataalamu mbalimbali nchini na hata maprofesa ambao
hawakusoma katika mfumo huo wakiwamo walimu wake (Ndalichako) waliosoma
kupitia mfumo huo.
Imeandikwa na Hellen Mlacky, Lucy Lyatuu na Regina Kumba.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment