Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Chuo
Kikuu cha Ardhi kimetoa zawadi na tuzo kwa wanafunzi 104 waliofanya
vizuri kitaaluma ili kutoa hamasa kwa wanafunzi wengine kuweka juhudi
katika masomo.
Zawadi
hizo zimetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa Chuo hicho,
Prof. Idrissa Mshoro ambaye ametangaza kuwa jumla ya wanafunzi wanne
kati ya waliofanya vizuri wamepata alama sawa hivyo kuibuka washindi wa
jumla kwa mwaka 2016.
Akisoma
hotuba wakati wa sherehe hizo, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho
(Taaluma), Prof. Gabriel Kassenga amesema kuwa sherehe hizo zimekuwa
zikiwezeshwa na wadau mbalimbali waliojitoa kwa hali na mali kutoa
zawadi na tuzo kwa wanafunzi waliofaulu vizuri kwenye vipengele
mbalimbali vya taaluma hivyo amewasihi wadau hao kuendelee kuunga mkono
jitihada zinazofanywa na wanafunzi hao ili kuwashawishi wanafunzi
wengine kufanya vizuri.
“Zawadi
mbalimbali zinazotolewa na wafadhili zimekua zikiwasaidia wanafunzi
hawa kuongeza tija kwenye maisha yao ya kielimu na kiuchumi kwani wengi
wao wamekuwa wakizitumia fedha hizo kama mitaji ya kufanyia biashara
pindi wamalizapo masomo yao,”alisema Prof. Kassenga.
Amefafanua
kuwa mwaka huu umekuwa wa tofauti kwani idadi ya wanafunzi wanawake na
wanaume waliopata tuzo hizo iko sawa tofauti na miaka mitatu iliyopita
ambapo wanawake walikua wakiongoza kwa asilimia 3.7 kwa kupata tuzo
nyingi wakati wanaume wakiwa ni asilimia 2.2.
Prof.
Kassenga ametaja baadhi ya zawadi zilizotolewa na wafadhili
walioshiriki katika shughuli hiyo kuwa ni vyeti, Kompyuta mpakato
(laptop),vifaa vinavyotumika katika kupimaji wa ardhi pamoja na fedha
taslimu.
Aidha,
Prof. Kassenga ametoa rai kwa kwa wanafunzi wote waliomaliza chuoni
hapo kuwa juhudi walizokuwa wakizionyesha wakati wa masomo waende
wakaziendeleze katika jamii zinazowazunguka pamoja na kwenye shughuli
mbalimbali za ujenzi wa Taifa ili wakawe mfano bora kwa vizazi vijavyo.
Kwa
upande wake Emily Elandogo ambaye ni mmoja kati ya wanafunzi waliopewa
zawadi hizo amewashukuru walimu wa chuo hicho kwa elimu wanayoitoa
ambayo itakua ni chanzo cha kuwaletea maendeleo sehemu yoyote
watakapokuwa pia ametoa ushauri kwa wanafunzi wenzake kuitumia vizuri
elimu waliyoipata ili iweze kuwasaidia katika maisha yao.
Mahafali
ya Kumi ya chuo hicho yanategemewa kufanyika Disemba 3 mwaka huu katika
viwanja va chuo hicho ambapo wahitimu wa shahada mbalimbali
watatunukiwa stahili pamoja na vyeti vyao.
MWISHO
CHUO CHA ARDHI CHATOA ZAWADI KWA WANAFUNZI 104 WALIOFAULU.
No comments:
Post a Comment