Na
Daudi Manongi
MAELEZO.
Dar
es Salaam
WAZIRI wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo
amekabidhi nyaraka za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 20 wa kitanzania
wanaokwenda kusoma fani za mafuta na gesi katika ngazi za uzamili na uzamivu
nchini China.
Watanzania hao 20
wamepatikana kutokana na mchujo na Wizara hiyo ukihusisha watanzania 89 kwenye
ngazi mbalimbali za elimu nchini.
Akizungumza wakati wa
kukabidhi nyaraka hizo leo Jijini Dar es Salaam, Prof. Muhongo alisema kuwa
wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikisomesha vijana wa kitanzania nje ya nchi
kwa ajili ya kusomea masuala ya mafuta na gesi.
“Serikali ya China
imetoa nafasi kwa vijana wa kitanzania kusoma nchini mwao na kwa jinsi ilivyo
tukaona ni vyema tuzitangaze nafasi hizi kwa Watanzania wote kupitia wizara
yetu ili waweze kuisaidia nchi yao na baada ya mchujo leo hii tunawakabidhi
nyaraka zao za masomo” alisema Profesa Muhongo.
Aidha Profesa Muhongo
aliwataka vijana hao kuitumia vyema nafasi waliyoipata na kuhakikisha wanasoma
kwa bidii kwani nchi inahitaji wataalamu wa kutosha katika sekta ya mafuta na
gesi ambayo inakua kwa kasi ya haraka nchini.
Kwa upande wake Naibu
Balozi wa China Nchini Bw.Gou Haodong amewaasa watanzania hao kusoma kwa bidii
wakiwa nchini china na kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kitaaluma.
Pia amewaasa
kuhakikisha wanawafundisha watu wa china utamaduni wa mtanzania na wawe
mabalozi wazuri wa nchi yao.
Serikali ya China
inatoa ufadhili wa nafasi 20 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitano kwa
watanzania ili kujifunza masuala ya Gesi na Mafuta nchini mwao kupitia Wizara
ya nishati na madini.
MWISHO
No comments:
Post a Comment