WABUNGE wameitaka serikali kuangalia
uwezekano wa kubadili uamuzi wake wa kuondoa misamaha ya kodi kwa
taasisi za dini, kwa kile walichosema ndizo zinazotoa huduma za afya
maeneo ambayo serikali haina zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Wakichangia mjadala wa bajeti ya 2016/17 bungeni mjini Dodoma jana, Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda, alisema serikali haijaweza kupeleka ipasavyo huduma za afya vijijini na hospitali zinazotoa huduma hizo ni za taasisi za dini, hivyo kuziwekea kodi ni kuwaweka wananchi katika mazingira magumu.
Alisema madhehebu ya dini yanatoa huduma na siyo kufanya biashara na wakati mwingine zimetoa huduma bure kwa wananchi maskini, jambo ambalo haliwezi kufanyika katika hospitali za serikali.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Aza Hilali, alisema serikali haijatekeleza azma yake ya kujenga vituo vya afya 3,963 kila kata kama ilivyoahadiwa na Rais wakati wa kampeni nab ado haijaeleza jinsi itakavyotekelezwa.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hilal, aliitaka serikali kuboresha huduma za afya, huku akieleza kuwa katika mkoa wa Rukwa taasisi ya Benjamini Mkapa imejenga majengo kwa ajili ya kutoa huduma za afya lakini yameshindwa kutumika kutokana na ufinyu wa bajeti katika sekta hiyo.
Mbunge wa Njombe Mjini (CCM), Edward Mwalongo, alisema ni vyema serikali ikaangalia upya suala la kuondoa msamaha wa kodi kwa taasisi za dini kwa kuwa waathirika wakubwa watakuwa wananchi wa kawiada kwani huduma za afya zitapanda bei mara dufu na za serikali ni duni.
Katika Bajeti ya mwaka huu, serikali imependekeza kufutwa kwa misamaha ya kodi inayotolewa kwa wafanyabiashara, watumishi wa umma, mashirika ya dini na taasisi zisizo za kiserikali.
Chanzo Gazeti la Nipashe
No comments:
Post a Comment