CHUO Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS), kimesema kitaanza
kutoa huduma za kliniki kwa wagonjwa wa selimundu katika hospitali za
mikoa nchini. Awali, huduma hizo zilizokuwa zikitolewa na Hospitali ya
Rufaa ya Muhimbili zilisitishwa baada ya kuzidiwa wagonjwa.
Mratibu wa magonjwa hayo kutoka MUHAS, Dk Deogratius Soka, alisema
kwa kuanzia tayari katika Hospitali ya Temeke kliniki imekamilika na
kuanza kutoa huduma na wanaendelea kuandaa katika hospitali za mikoa za
Amana na Mwananyamala jijini Dar es Salaam kisha kwenda mikoa mingine.
“Huduma za kliniki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),
hazikusitishwa bali zilipotoshwa kwani wingi wa wagonjwa ulifanya
tutawanye huduma mikoani kwa kuanza kufanya kliniki na Muhimbili
kubakisha wagonjwa wanaohitaji msaada zaidi,” alisema.
Alisema, kwa kawaida watu wenye ugonjwa huo wanatakiwa kuonana na
madaktari katika kliniki zao maalumu kila baada ya miezi mitatu, lakini
katika Hospitali ya Muhimbili walikuwa wakifika kila baada ya zaidi ya
mwaka kutokana na wingi wa wagonjwa.
Dk Soka alisema, katika ujenzi wa maandalizi ya kliniki hizo
wataangalia maeneo yenye wagonjwa wengi zaidi na kisha kuendelea mikoa
mingine kutokana na kuwa serikali wameuingiza ugonjwa huo katika
magonjwa yasiyoambukizwa hivyo kusamehewa katika matibabu au kuchagia
kidogo.
Alisema, mikoa ya ukanda wa Pwani kama Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es
Salaam pamoja na ile ya Kanda ya Ziwa kama Mwanza ,Shinyanga na
mingineyo ndiyo inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wenye ugonjwa
huo.
Alisema Tanzania ni nchi ya tano duniani kwa watu wake kuwa na
ugonjwa huo wakifuatiwa na India, Nigeria, Congo na Algeria, hivyo
ugonjwa huo kuwa na athari kubwa katika jamii kutokana na uelewa mdogo.
Alisema, baadhi ya watu wana imani potofu kuwa watoto wenye ugonjwa
huo hawawezi kuishi zaidi ya miaka 18, jambo analoeleza kuwa si kweli.
Pia, alisema upotoshaji mwingine ni kwamba mtoto mwenye ugonjwa huo
akifikisha umri wa miaka hiyo 18 hupona. Anafafanua kuwa anayepata
ugonjwa huo huishi nao kwa miaka yote na ana uwezo wa kuwa hai mpaka
kufikia uzee.
No comments:
Post a Comment