Social Icons

Thursday 16 June 2016

MADUDU YA KUTISHA NDANI YA BODI YA MIKOPO YAANIKWA

Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Tumieni mtandao huu ni wenu nyote. 


Kutokana na kubainika kwa madudu hayo, serikali imetoa wiki mbili kwa wahusika wa madudu hayo, kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mkaguzi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia na Mafunzo ya Ufundi, amefichua madudu hayo yakiwamo kutokuingizwa katika mfumo wa kumbukumbu malipo ya Sh. milioni 270.894 ya wanafunzi 247 waliofanya marejesho, wanafunzi 262 kulipwa Sh. bilioni 10.782 huku kumbukumbu zikionesha wanatakiwa kurejesha Sh. bilioni 5.535.
Mengine ni kuwapo kwa wanafunzi wanufaika na mikopo kutoka HESLB na wakati huohuo wakipokea mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar (ZHESLB), kuwapo kwa wanafunzi 105,202 ambao hawajarejesha mkopo wa Sh. bilioni 712.872 toka mwaka 1994 hadi 2013.
Pia wanafunzi 2,619 waliotakiwa kurejesha mkopo wa Sh. bilioni 14.468, majina yao yametokea katika vyuo viwili huku wakitumia namba moja ya kidato cha nne. Wanafunzi hao walikopeshwa Sh. bilioni 7.126 katika chuo cha kwanza na Sh. bilioni 7.341 katika chuo cha pili.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, aliyasema hayo jana wakati akitoa taarifa ya mkaguzi aliyefanya kazi hiyo katika bodi, baada ya watendaji wakuu wa HESLB kusimamishwa kazi Februari 16, mwaka huu, kupisha uchunguzi.
Prof. Ndalichako aliwasimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, George Nyatega na wakurugenzi wengine watatu kutokana na utendaji mbovu katika kuendesha bodi hiyo.
Wengine waliosimamishwa kupisha uchunguzi ni Mkurugenzi wa Mikopo ya wanafunzi, Mkurugenzi wa Urejeshaji wa Mikopo, Mkurugenzi Upangaji na Utoaji wa Mikopo.
Akizungumzia matokeo ya uchunguzi huo, Prof. Ndalichako alisema wamebaini kulikuwapo na wanafunzi walionufaika na mikopo ya HESLB huku pia wakipokea mkopo kutoka ZHESLB.
“Kwa mfano wanafunzi 262 walinufaika na mikopo ya Sh. bilioni 10.782 lakini kumbukumbu zinaonyesha wanatakiwa kurejesha Sh. bilioni 5.535. pia wanafunzi 247 walifanya marejesho ya mikopo ya awali kwa kiwango cha asilimia 25 na walilipa Sh. milioni 270.8 lakini hawakuingizwa kwenye orodha ya waliorejesha,” alisema.
Alisema pia walibaini kuwapo kwa upungufu katika malipo ya mikataba ya utammbuaji na ukusanyaji wa madeni, na kwamba wanufaika 462 walitambuliwa na wazabuni tofauti na kuwasilishwa HESLB wakiwa na kiasi kikubwa cha mkopo kuliko mkopo wao halisi wa Sh.bilioni 2.842, huku deni lililoonyeshwa likiwa ni Sh. bilioni 3.670.
Alisema kuwapo kwa ongezeko la Sh. milioni 828.348 linafanya kamisheni kuwa kubwa, alisema wazabuni tofauti wamekuwa wakilipwa kamisheni kwa kutambua watu wanaofanana.
“Kampuni zilizopewa jukumu la kukusanya madeni zilikuwa na majina ya ajabu ajabu, mfano Machomengi, tukaenda Brela (Wakala wa Usajili wa kampuni) halipo kwenye usajili, zingine zilikuwa kampuni za uuzaji wa vifaa vya ujenzi mfano mwingine ni kampuni kama Sikonge, kwa hiyo kulikuwa na ubabaishaji mkubwa,” alisema.
KUHUSU NACTE
Prof. Ndalichako alisema walifanya uchunguzi katika Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) na kubaini udhaifu katika usimamizi wa mafunzo yanayotolewa vyuoni kwa kutokuwa na wataalamu wa kutosha wenye sifa stahiki za kusimamia ukuzaji na uboreshaji mitaala. Pia wafanyakazi kupangiwa majukumu bila kujali ujuzi walionao.

“Kwa mfano aliyesomea masuala ya utumishi amepangiwa kusimamia ukuzaji na uboreshaji mitaala, pia kutotilia mkazo suala la ufuatiliaji wa ubora wa elimu inayotolewa katika vyuo wanavyovisimamia, mwaka 2014/15, Nacte ilikusanya Sh. bilioni 1.568 lakini ilitumia Sh.milioni 174.166 kwa ajili ya kudhibiti ubora wa elimu,” alisema.
Alisema Nacte imeweka sifa ya chini kwa wanafunzi kujiunga na vyuo, alisema mitaala inayopitishwa na Nacte hugeuzwa kuwa mali yake badala ya chuo husika, kutokana na kujimilikisha mitaala hiyo, Nacte wamekuwa na mamlaka ya kuigawa kwa vyuo vingine bila idhini ya chuo husika.
HATUA ZILIZOCHUKULIWA
Prof. Ndalichako alisema HESLB inapaswa kupitia dosari zote na kuchukua hatua mara moja kwa wahusika wote, kuhakikisha mfumo wa utoaji mikopo unalinganishwa na mfumo wa urejeshaji, HESLB kufuatilia wadaiwa wote na kuanza kwa makato mara moja,

Maagizo mengine ni kuwafuatilia wanafunzi 2,619 waliopewa mikopo kwa kutumia namba za kidato cha nne zinazofanana na kuhakikisha fedha walizochukua katika vyuo viwili tofauti zinarejeshwa, kutoa maelezo kuhusu wanafunzi 168 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliokopeswa Sh. milioni 531.323 na wanafunzi 919 wa Chuo Kikuu cha Dodoma waliokopeshwa Sh. bilioni 2.530 na hawakuweza kutambuliwa na vyuo hivyo fedha hizo zimerejeshwa HESLB.

Chanzo Gazeti la Nipashe
 

No comments: