Social Icons

Thursday 14 January 2016

Tshs 459/- bn zawanufaisha wanafunzi 122,486 elimu ya juu 2015/2016

Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Tumieni mtandao huu ni wenu nyote. 


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa jumla ya Tshs 459/- bilioni  kama mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi 122,486wanasoma katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi katika mwaka wa masomo 2015/2016. 
Hii ni idadi kubwa zaidi ya wanufaika na fedha kuwahi kutolewa tangu kuanzishwa kwa Bodi mwezi Julai, 2005 na kwa ujumla, katika historia ya utoaji wa mikopo nchini. Fedha hizi zimetolewa kati ya mwezi Novemba, 2015 na Januari 10, 2016.   
Katika mwaka uliopita wa masomo, 2014/2015, Serikali kupitia Bodi ilitoa jumla ya Tshs 341/- bilioni zilizowanufaisha wanafunzi 99,069.
Kati ya fedha zilizotolewa, jumla ya Tshs 199.7 bilioni zinakwenda kwa wanafunzi 53,537waliojiunga na masomo kwa mwaka wa kwanza mwezi Novemba, 2015 katika vyuo mbalimbali na Tshs Tshs 259.1 bilioni zinalipwa kwa wanafunzi68,916 wanaoendelea na masomo, yaani mwaka wa pili, wa tatu na kuendelea katika vyuo vya umma na binafsi. 
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam leo (Jumatano, Januari 13, 2016), kundi kubwa katika ya wanafunzi waliopata mikopo ni wale wanaosoma programu za kipaumbele ambazo zimetajwa katika mwongozo (Guidelines) uliotolewa na Bodi mwezi Mei mwaka jana, 2015. 
Programu hizo ni Udaktari wa Binadamu, Udaktari wa Meno, Udaktari wa Wanyama, Ufamasia na Uuguzi na Ualimu wa Masomo ya Sayansi na Hesabu na Uhandisi wa Umwagiliaji. Wanufaika wengine ni yatima na walemavu.
Katika hatua nyingine, Bodi ya Mikopo inatoa wito kwa waajiri katika taasisi za umma na binafsi nchini kuhakikisha wanazingatia matakwa ya sheria iliyoanzisha Bodi inayowataka kuwatambua waajiriwa wao ambao ni wanufaika wa mikopo inayotolewa na Bodi; kukata sehemu ya mishahara yao na kuwasilisha kwa bodi kama marejesho. 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Bodi, Kifungu cha 20 (1) (c) cha sheria ya iliyoanzisha Bodi (Higher Education Students’ Loans Board Act (as amended)), kinawataka waajiri kuwatambua waajiriwa, kuijulisha Bodi kwa maandishi ndani siku 28 tangu wapate ajira. Aidha, Kifungu cha 20 (2) cha sheria hiyo, kinawataka waajiri, baada ya Bodi kuthibitisha kuwa muajiriwa ni mnufaika wa mikopo ya Bodi, (mwajiri) kuitaarifu kuitaarifu Bodi, ndani ya siku 30 za ajira yake na kukata makato kutoka katika mshahara wa mwajiriwa na kuyawasilisha Bodi ndani ya siku 15 baada ya kila mwisho wa mwezi.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa waajiri wote wanapaswa kutimiza matakwa hayo ya kisheria na kuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameanza kukagua taaasisi za umma kama zinazingatia matakwa haya ya kisheria.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005. Bodi ina majukumu kadhaa, lakini mawili makubwa ni kutoa mikopo kwa wanafunzi watanzania wahitaji; na kusimamia urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika wa mikopo.

Imetolewa na;
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU
Jumatano, Januari 13, 2016
DAR ES SALAAM


No comments: