Social Icons

Monday 5 May 2014

MWENYEKITI WA JUMUIYA YA VYUO VIKUU TANZANIA ASIMAMISHWA WADHIFA HUO.


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk.Shukuru Kawambwa.
Mkutano  wa marais wa Jumuiya ya Vyuo Vikuu Tanzania (Tahliso), umemsimamisha Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Leonard Mdede, baada ya kudaiwa kukiuka katiba ya jumuiya kutokana na kujihusisha na masuala ya kisiasa.
Maamuzi hayo yalifikiwa jana katika mkutano mkuu wa Tahliso uliofanyika jijini Dar es Salaam katika Chuo cha Kodi kwa siku mbili kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wa vyuo vikuu.

Makamu Mwenyekiti wa Tahliso, Abdi Mahamoud, alisema wamechukua uamuzi huo kutokana na mwenyekiti wa Tahliso kujihusisha na masuala ya kisiasa kwa kugombea ubunge katika hatua ya kura za maoni kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa.

“Kwa mujibu wa katiba ya Tahliso, ni marufuku kwa rais au mwenyekiti wa jumuiya hiyo kujihusisha na masuala ya siasa na kuchukua uamuzi wa kugombea nafasi za kisiasa kupitia chama chochote cha siasa,ndiyo maana tumemsimamisha,” alisema.

Alisema inapobainika kiongozi ndani ya Tahliso anajihusisha na masuala ya kisiasa jamii haiwezi kuielewa jumuiya hiyo ambayo lengo lake kuu ni kuboresha elimu katika vyuo vikuu nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Seneti, Eshe Mzee, alisema baada ya kumsimamisha mwenyekiti huyo, watapeleka muhtasari wa mkutano huo uliotoa maamuzi hayo kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kwa maamuzi ya mwisho kwa sababu Tahliso ipo chini ya wizara hiyo.

Mdede akizungumzia tuhuma zilizoelekezwa kwake, alisema hazina msingi na kwamba maamuzi yaliyofikiwa katika kikao kilichohamia Chuo cha Ustawi wa Jamii kutoka Chuo cha Kodi siyo halali kwa sababu hakuwapo.

“Maamuzi yaliyofikiwa siyo halali, walitaka kunisimamisha wakati mkutano unafanyika Chuo cha Kodi, lakini polisi wakaja wakaingilia kati kutokana na hali ya usalama kutokuwa nzuri, kwa hiyo hawajanisimamisha,” alisema Mdede.

Wakati wa mkutano huo, Mdede pia alituhumiwa kwamba tangu achaguliwe mwezi Desemba mwaka jana hajaitisha kikao cha viongozi wa vyuo kama taratibu na sheria za Tahliso zinavyoelekeza.

Taarifa kutoka ndani ya mkutano huo zinaeleza kuwa Mdede baada ya kutuhumiwa kwa makosa hayo alikiri na kuomba radhi wajumbe.

Hata hivyo, kabla ya kusoma maamuzi ya kumsimamisha mwenyekiti huyo, ghafla walifika askari wakiwa katika gari KX 06 EFY na kuwaamuru marais wa vyuo hivyo kusitisha mara moja kuendelea na mkutano huo.

Marais hao walitii amri na kuhamia katika ukumbi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii kutoka Chuo cha Kodi ambako walikwenda kusoma maamuzi ya kumsimamisha mwenyekiti wao.
 
CHANZO: NIPASHE    

No comments: