Mkuu
wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI), Bi. Zuki Njalai Mihyo
(aliyesimama) akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu juu
ya masuala ya Jinsia, Demokrasia na Katiba Mpya yalioandaliwa na GTI.
MKUU
wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI), Bi. Zuki Njalai Mihyo leo jijini
Dar es Salaam amefungua mafunzo ya siku tatu juu ya masuala ya Jinsia,
Demokrasia na Katiba Mpya yaliyowashirikishwa washiriki kutoka katika
mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Pwani na Morogoro.
Akizungumza
katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika
Chuo cha Mafunzo ya Jinsia kilichopo eneo la Mabibo jijini Dar es
Salaam, Bi. Zuki Mihyo alisema kutokuwepo na misingi imara ya kutetea,
kulinda na kudumisha demokrasia iliyojengwa kwenye misingi ya usawa wa
kijinsia inayo tambulika Kikatiba kumechangia uwepo wa tatizo la
unyanyasaji wa kijinsia nchini.
Alisema
tatizo la unyanyasaji wa kijinsia licha ya kuwapata watu wa jinsia
zote, limekuwa likiwaathiri zaidi wanawake na watoto wa kike tofauti na
ilivyo kwa wanaume na watoto wa kiume katika jamii, hivyo kushauri kuna
kila sababu ya kupambana na mifumo kandamizi inayochangia hali hiyo.
“…Wanawake
na watoto wa kike mara nyingi wamekuwa wakifanyiwa ukatili huu na
wanaume au wavulana ambao wanaweza kuwa ndugu zao wa karibu, marafiki na
hata wenzi wao,” alisema Mkuu huyo wa chuo cha GTI kilichopo chini ya
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)
Alisema
suala la ukekelezaji wa mila na desturi kama vile ukeketaji, kurithi
wajane na mila nyingine nyingi zinazowagandamiza wanawake na makundi ya
pembezoni na kuwafanya kutokuwa na sauti wala kushiriki katika kutoa
uamuzi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa vimekuwa vikichangia ukatili
wa jinsia kwa wasichana, wanawake na makundi mengine ya pembezoni.
“…Tunaelewa
kuwa wakati wa zamani mila nyingi zilikuwa na maana lakini kwa wakati
huu mila hizo zimepitwa na wakati hivyo ziachwe ili kukomesha dhuluma,
manyanyaso, ukandamizaji n.k, ili kuwa na usawa kwa watu wote,” alisema.
Aidha
alifafanua kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa
washiriki kuweza kushiriki katika kuchambua masuala ya jinsia,
demokrasia na katiba mpya ili waweze kuyasimamia na kuyatetea katika
mikakati mbalimbali ya maendeleo. Aliongeza kuwa malengo mahususi ni
pamoja na kukuza uelewa na utambuzi wa uhusiano baina ya dhana za
jinsia, demokrasia na katiba, kuchochea ushiriki na uwajibikaji wa asasi
za kiraia na makundi maalumu yaliopo pembezoni na mchakato wa
kidemokrasia na kutambua changamoto na fursa zilozopo katika kuingiza
masuala ya jinsia na demekrasia kwenye katiba mpya.
Akifafanua
zaidi juu ya mafunzo hayo, mmoja wa watoa mada, Geoffrey Chambua
alisema washiriki wanatoka katika ngazi ya jamii; yaani katika asasi za
kiraia, vikundi vya kijamii, asasi za kidini, wajasiliamali na makundi
maalumu wote kutoka katika mikoa ya Morogoro, Lindi, Pwani pamoja na Dar
es Salaam yenyewe. Chambua alisema mafunzo kama hayo pia yanaendelea
katika kanda anuai.
No comments:
Post a Comment