Social Icons

Thursday, 5 October 2017

TCU WAFUNGUA TENA UDAHILI VYUO VIKUU

Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. insta : @matukionawanavyuo Tumieni mtandao huu ni wenu nyote. 

Imeandikwa na Mwandishi Wetu
Jengo la Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kufungua maombi kwa awamu ya pili ya udahili wa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na masomo ya shahada za awali kwa mwaka wa masomo wa 2017/18, baada ya kubainika waombaji wengi hawakuchaguliwa kutokana na sababu mbalimbali.
Awamu ya kwanza ya udahili huo ilimalizika tangu Agosti 30, mwaka huu na uhakiki wa majina ya waombaji wanaotaka kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kukamilika. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Profesa Eleuther Mwageni jana, awamu hiyo ya pili ya maombi ya udahili inaanzia rasmi tangu jana na itakamilika Oktoba 10, mwaka huu.
Profesa Mwageni alisema tume hiyo imechukua hatua hiyo ya awamu ya pili ya udahili ili kuruhusu udahili kwa waombaji waliokosa nafasi kwenye awamu ya kwanza, waombaji wa kidato cha sita walioshindwa kuomba awamu ya kwanza na waombaji wenye vigezo vya Stashahada walioshindwa kupata namba ya uhakiki wa tuzo (AVN).
Aidha, alitaja sababu nyingine za awamu hiyo ya pili ya udahili kuwa ni kuruhusu udahili kwa waombaji waliomaliza mitihani ya Cambridge mwaka huu na matokeo yao yameshatoka na wanafunzi wa vyuo vikuu watakaokuwa na uthibitisho kutoka vyuo vya awali.
Kwa mujibu wa ratiba ya TCU, kwa sasa iko katika hatua kutangaza udahili wa wanafunzi watakaojiunga na vyuo vya elimu ya juu, hatua iliyokamilika Oktoba 2, mwaka huu. Baada ya hapo, ratiba hiyo imeonesha kuwa imetoa muda kwa ajili ya wanafunzi wanaoomba uhamisho, utaratibu utakaochukua muda wa siku 20 na kukamilika rasmi Novemba 30 kupisha uhakiki wa wanafunzi waliodahiliwa kwenye vyuo vyote vya elimu ya juu nchini utakaofanyika Desemba Mosi, mwaka huu.
Hata hivyo, hivi karibuni mwaka huu TCU ilitangaza kubadili mfumo wa udahili ambapo kuanzia mwaka 2017/18 maombi ya kujiunga na elimu ya juu yanatumwa moja kwa moja vyuoni. TCU imepanga Oktoba 30, mwaka huu kuwa siku ya kufunguliwa kwa vyuo vyote vinavyotoa elimu ya juu.
Kwa mujibu wa Profesa Mwageni, Tume hiyo haitopokea maombi ya kujiunga na vyuo vikuu kama ilivyokuwa hapo mwanzo na kwamba utaratibu wa kutuma maombi ni ule ule uliotumika katika awamu ya kwanza ya udahili.
April 15, mwaka huu, wakati akizindua hosteli za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais John Magufuli aliiagiza TCU kutowachagulia vyuo wanafunzi wa elimu ya juu na kuwaacha wajichagulie wenyewe vyuo wanavyovitaka.
CHANZO HABARI LEO

No comments: