Social Icons

Monday 4 September 2017

RITA YAWAONGEZEA MUDA WANAFUNZI KUHAKIKI VYETI

Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. insta : @matukionawanavyuo Tumieni mtandao huu ni wenu nyote. 
 Imeandikwa na Mwandishi Wetu
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umeongeza muda wa kupokea maombi ya uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kwa wanafunzi wanaoomba mikopo ya masomo ya elimu ya juu mwaka 2017/2018 hadi Septemba 7, mwaka huu.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson alisema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari, na kuwataka waombaji wote wa mikopo ya masomo ya elimu ya juu ambao hawajawasilisha vyeti vyao kwa ajili ya kuhakikiwa wahakikishe wanatuma maombi ndani ya muda huo.
“Baada ya tarehe hiyo ofisi itashughulikia maombi yaliyotumwa kwa njia ya barua pepe au kuwasilishwa moja kwa moja katika ofisi zetu zilizopo kwa wakuu wa wilaya na Rita Makao Makuu na kutoa majibu kwa waombaji,” alisema Hudson.
Pia alisema wananchi waliotuma maombi yao kwa njia ya barua pepe wanaendelea kujibiwa na wale waliowasilisha katika ofisi yao Makao Makuu jijini Dar es Salaam wafike. Wiki iliyopita, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) iliongeza muda wa siku saba kuanzia Septemba 4, 2017 hadi 11, mwaka huu ili waombaji wenye sifa wawasilishe maombi yao kabla ya kufungwa kwa dirisha la maombi.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema hadi kufikia wiki iliyopita, jumla ya waombaji wa mikopo kwa njia ya mtandao walikuwa 49,282, kati yao waombaji 15,473 wakiwa wamekamilisha maombi yao kwa njia ya mtandao kwa kufuata taratibu zote za uombaji zilizotolewa na Bodi.
Alisema kwa takwimu za maombi hayo, wapo waombaji 33,809 ambao wapo katika hatua mbalimbali za kuambatanisha nyaraka zao za maombi na kuwataka wale ambao hawajakamilisha kuwasilisha maombi yao ya mikopo kama ilivyoelekezwa.
Alisema waombaji wa mkopo wanatakiwa kuambatanisha nyaraka zao kwenye mfumo wa mtandao wa maombi hayo (OLAMS) kukiwa na nyaraka zilizosainiwa na viongozi wa serikali za mitaa na makamishna a viapo au Hakimu na kuziweka katika mtandao huo.
Hatua mojawapo ni kuwa na nakala ya cheti cha kuzaliwa kilichothibitishwa na Rita na kama muombaji atakuwa yatima, awasilishe nakala ya cheti cha kifo kilichothibitishwa na Rita. “Iwapo muombaji alifadhiliwa, awasilishe nakala ya barua kutoka taasisi iliyofadhili masomo na nyaraka nyingine muhimu zinazothibitisha uhitaji wa muombaji,” alieleza Badru.
CHANZO HABARI LEO

No comments: