Imeandikwa na Lucy Ngowi
UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, moja ya vyuo vikongwe na
vyenye heshima kubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki, umesema una
mikakati mingi ya kukifanya kuendelea kuwa bora ndani ya Ukanda husika,
Afrika na duniani kwa ujumla, ili kiendelee kuwa daraja la kielimu.
Aidha, kimesema kama kilivyotoa wasomi bora wanaoendelea kushika
nyadhifa mbalimbali ndani na nje ya Afrika, bado kinaendelea na
kitaendelea kutoa wasomi walioiva kwa soko la ajira.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma kwa Umma wa chuo hicho, Dk
Mona Mwakalinga. “Chuo Kikuu Dar es Salaam kinazalisha viongozi
wanapotoka hapa, ndiyo maana kimetoa marais wa nchi mbalimbali, mawaziri
wakuu, wakuu wa taasisi za kimataifa, na wengine wengi, hakika orodha
ni ndefu.
“Hiki ni chuo pendwa Tanzania na Afrika Mashariki, ni sehemu ambayo
ni chaguo la kwanza la wanafunzi kabla ya kuomba vyuo vingine,” alisema
Dk Mwakalinga aliyeongeza kuwa, chuo kina Kurugenzi ya Ushirikiano wa
Kimataifa ambayo inahakikisha inakiuza chuo ndani na nje ya nchi ili
kipate walimu na wanafunzi.
Amesema mwanafunzi anapomaliza masomo yake chuoni hapo anaweza
kuuzika katika nchi za Afrika Mashariki na ulimwenguni pote. Dk
Mwakalinga alisema hayo alipokuwa akizungumza na Habari Leo kuhusu
uhusiano wa chuo hicho na wanafunzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
wanaomaliza chuoni hapo.
Alisema mwanafunzi yeyote anayetoka UDSM, anaweza kwenda vyuo vikuu
vya Nairobi nchini Kenya ama Kampala nchini Uganda na kuendelea na
masomo yake. “Katika Afrika Mashariki tuna umoja wa kushirikishana
wanafunzi na walimu.
UDSM tunatoa taaluma ambayo mtu akitoka chuoni hapa anaweza kwenda
Nairobi kuendelea na masomo,” alisema na kuongeza kuwa pia kinamsaidia
mwanafunzi anayesoma hapo kuuzika Afrika Mashariki na kwingineko.
Alisisitiza kuwa chuoni hapo milango ipo wazi kwa wanafunzi wote, pia
kuna walimu wanatoka hapo na kwenda kufundisha vyuo vingine vya Afrika
Mashariki na walimu wa nchi za Afrika Mashariki wanakuja chuoni hapo
kufundisha.
Alisema chuo kimekuwa kinapokea wanafunzi kutoka Kenya, Uganda,
Burundi na nchi nyingine zenye makubaliano maalumu, ikiwemo Angola. Chuo
hicho, kimetoa marais, wakiwemo Jakaya Kikwete aliyeiongoza Serikali ya
Awamu ya Nne Tanzania, na Dk John Magufuli, rais wa sasa.
Wengine ni Yoweri Museveni wa Uganda, Rais wa zamani wa Benki ya
Maendeleo Afrika (AfDB), DK Donald Kaberuka ambaye ni raia wa Rwanda,
Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Kenya, Willy Mutunga, John Garang, Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Sudan.
Pia kimetoa Mawaziri wakuu wanne wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliyepo
madarakani, Joseph Warioba, Mizengo Pinda na Edward Lowassa. Aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha Rose-Migiro pia ni
miongoni mwa matunda ya UDSM, kama ilivyo kwa Eriya Kategaya, Naibu
Waziri Mkuu wa Uganda aliyekuwa pia Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki. Orodha ni ndefu, lakini UDSM kinaahidi kuendelea kuibua
wasomi na watendaji katika taasisi mbalimbali zenye kiwango cha
kimataifa.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment