Wanafunzi 20 kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini wamepata ufadhili wa elimu unaofikia jumla ya Tshs Milioni 70 kutoka Klabu ya Rotary ya Oyster Bay, fedha zilizokusanywa kutokana na michango ya makampuni na watu binafsi.
Lengo la mradi huu ni kutoa msaada wa kifedha kwa wanafunzi wa Kitanzania wenye alama za juu kimasomo na waliopata nafasi za kujiunga na vyuo lakini wakakosa fedha za kulipia masomo.
Wanafunzi hao walikabidhiwa hundi za malipo katika tafrija fupi iliyofanyika tarehe 18 November katika mgahawa wa Waterfront uliopo Slipway jijini Dar es Salaam. Tafrija hiyo iliandaliwa kwa lengo la kuadhimisha miaka 100 ya mfuko wa Rotary ambapo fedha zilizochangishwa katika hafla hiyo zitawekwa kwenye mfuko huo wa Rotary ujulikanao kama Rotary Foundation.
Rotary Foundation iliyoanzishwa miaka 100 iliyopita ina lengo la kuwawezesha wanachama wa Rotary duniani kote kukuza amani kwa kuboresha afya, kusaidia elimu na kutokomeza umasikini. Mradi wa Klabu ya Rotary Oyster Bay wa ufadhili wa masomo unaenda sambamba na juhudi za Rotary International za kusaidia elimu.
Mradi wa ufadhili wa masomo katika Klaby ya Rotary ya Oyster Bay ulianza mwaka 2010 na wanafunzi wawili kwa msaada wa mfadhili mmoja. Katika kipindi cha miaka mitano, mradi huu umefanikiwa kuwa mradi mkubwa zaidi ukilinganisha na miradi mingine inayofanywa na klabu hiyo. Mwaka huu, klabu ya Rotary ya Oyster Bay imetoa ufadhili kwa wanafunzi 20 kwenye aina mbalimbali za masomo ikiwemo uhasibu, uhandisi, udaktari na sheria na inajivunia kuanza kuona matunda yake ambapo mmoja wa wanafunzi hao amehitimu na kuanza kazi ya udaktari.
Wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini Tanzania hutuma maombi ya ufadhili na mchakato wa kina hufanyika ili kuchagua wanafunzi wanaokidhi vigezo. Maendeleo ya wanafunzi wanaochaguliwa kupata ufadhili huangalia kwa ukaribi ili kubaini kama wanastahili kuendelea kupata ufadhili wa masomo katika mwaka unaofuata.
Mradi huu wa ufadhili Kwa wanafunzi unawezeshwa na michango kutoka kwa makampuni na watu binafsi ambapo mwaka huu michango imetoka Karimjee Scholarships, Karimjee Jivanjee Scholarships, D.B Shapriya Scholarships, R Sheth Scholarships, K Shah Scholarships, Nasim Manji, JDC Scholarships, Eleanor and Paul Best, Diamond Trust Bank, S Rhemtullah, pamoja na Gajjar Autoworks and Premium Finishes Limited.
No comments:
Post a Comment