Social Icons

Monday 7 March 2016

UDSM YAKANA KUWANYANYASA WATUMISHI WAKE.

Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Tumieni mtandao huu ni wenu nyote. 


Na. Aron Msigwa - MAELEZO.


Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umekanusha  tuhuma zilizotolewa na baadhi ya wafanyakazi waendeshaji wa chuo hicho kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuwa unaendesha vitendo vya dhuluma, uonevu na upendeleleo katika ulipaji wa mishahara na kuwasahau watumishi hao  jambo linalokwamisha ufanisi wa chuo hicho.

Taarifa ya kanusho dhidi ya tuhuma hizo iliyotolewa na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Utawala na kusainiwa  na Prof.Preksedis Marco Ndomba leo jijini Dar es salaam imeeleza kuwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kinaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Utumishi Umma nchini na kamwe hakina mamlaka ya  kumwonea, kumdhulumu wala kutoa upendeleo kwa mtumishi yeyote kwa kuwa suala hilo liko nje ya misingi iliyoanzisha chuo hicho.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kama ilivyo kwa vyuo vingine vya umma suala la maslahi hasa nyongeza za mishahara na marupurupu mengine ya watumishi wa vyuo hususan Chuo Kikuu cha Dar es salaam linapangwa na kuidhinishwa na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na siyo uongozi wa chuo hicho.

Aidha, mishahara ya watumishi wa chuo hicho hupangwa kulingana na kanuni na taratibu za Serikali na kuongeza kuwa wanataaluma wa Chuo hicho hupewa mishahara yao kutokana na Muundo wa Pamoja wa Utumishi wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu vya Umma wa mwaka 2014 na Sheria ya Kazi na mahusiano kazini ya mwaka 2004 na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009.

Kuhusu tuhuma za kuwepo kwa tofauti ya mishahara miongoni mwa watumishi wa Chuo hicho imeeleza kuwa hilo inatokana na tofauti ya vyeo waliyonayo watumishi hao na kuongeza kuwa wao kama viongozi wa chuo hicho hawana mamlaka ya kuwapangia mishahara watumishi wala kutengeneza nyaraka za mishahara.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam hupokea nyaraka za mishahara kwa watumishi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuzitekeleza na kuwataka watumishi hao kutambua kuwa tofauti ya vyeo waliyo nayo inawafanya walipwe mishahara tofauti.

Kupitia taarifa hiyo uongozi wa chuo hicho umeeleza kuwa hakuna upendeleo katika nafasi  za uongozi chuoni hapo kwa kuwa nafasi zote hujazwa kwa kufuata hati idhini ya chuo, pia hupatikana  kwa kushindanishwa kwa waombaji kwa sifa zao na inapotokea mtumishi katika nafasi ya Mkurugenzi uendeshaji anastaafu kazi  Menejimenti ya chuo humwomba mwanataaluma kutoka chuoni hapo kukaimu nafasi hiyo wakati taratibu za kuitangaza nafasi hiyo ili kumpata mkurugenzi mpya zikiwa zinaendelea.

Kwa upande wa tuhuma ya kuwepo kwa matumizi mabaya ya mali za chuo hasa magari kwa safari zisizohusiana na chuo hicho imefafanua kuwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kina Sera, Kanuni na miongozo mbalimbali inayodhibiti matumizi ya magari na mali za umma ikiwemo ujazaji wa vitabu maalum vya makabidhiano ya magari " Log Book".

Taarifa imebainisha kuwa UDSM hudhibiti matumizi ya magari yake  kwa  kuyawekea maandishi ubavuni na kwamba magari  hutakiwa kuegesha chuoni baada ya matumizi saa 12 jioni na wafanyakazi wanaoyatumia kinyume na miongozo iliyowekwa wanachukuliwa hatua za kinidhamu.

Aidha, ili kuboresha maslahi ya watumishi wa chuo hicho hasa upandishwaji wa vyeo ndani ya chuo muundo wa Utumishi wa wafanyakazi waendeshaji hutumika pia maboresho hufanyika kupitia vikao rasmi vya ajira kulingana na matakwa ya sheria ya kazi.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa Menejimenti ya chuo hicho baada ya kubaini kuwepo kwa changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa muundo wa Utumishi wa Waendeshaji iliamua kuuhuisha na kuuwasilisha kwa Msajili wa Hazina ili ufanyiwe kazi.

Pia kikao cha Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es salaam kilichofanyika Februari 12, 2016 pamoja na mambo mengine kilielekeza Chama cha Wafanyakazi UDSM kwa kushirikiana na Uongozi wa chuo kuandika muhtasari unaoaininisha changamoto za watumishi zilizopo ili ziwasilishwe katika Ofisi ya Msajili wa Hazina.

No comments: