Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Tumieni mtandao huu ni wenu nyote.
Na Anna Nkinda – Kuala Lumpur,
Malaysia
Chuo kikuu cha
Binary cha nchini Malaysia kimetoa nafasi 10 za ufadhili wa masomo ya shahada
ya Uzamili na Uzamivu katika fani za Ujasiriamali na Teknolojia ya Habari kwa
kipindi cha miaka mitatu kwa watanzania wataohitaji kusoma nchini humo.
Utiaji saini wa
makubaliano ya nafasi hizo za masomo zinazojulikana kwa jina la Binary - First Lady of Tanzania Scholarship Award umefanyika leo katika chuo hicho kati ya
Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Daud Nasibu na Mwanzilishi
na Mwenyekiti Mtendaji wa chuo hicho Prof. Joseph Adaikalam na kushuhudiwa na
Mke wa Rais Mhe. Mama Salma Kikwete.
Akiongea wakati wa hafla
hiyo ya utiaji saini Mke wa Rais Mhe. Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi
ya WAMA alikishukuru chuo hicho kwa kutoa nafasi 10 za masomo ambazo zitasaidia
sio tu kwa wataofaidika nazo moja kwa moja bali pia kwa jamii ambako wahitimu
watarejea kuitumikia.
Mhe. Mama Kikwete alisema kupitia mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) kwa upande wa elimu ya msingi na
sekondari Tanzania imelenga kujenga uwezo wa walimu kwa kutoa mafunzo ya pahala
pa kazi, kusaidia watoto wasiofanya vizuri kwa kuandaa vitendea kazi mahsusi
vinavyozingatia umri na mahitaji, kuboresha miundo mbinu kwa kujenga madarasa,
maabara na nyumba za walimu, kuboresha vifaa vya ufundishaji kama vile
madawati, vifaa vya maabara, vitendanishi (Kemikali) na uongeza motisha kwa
walimu.
“Mipango niliyotaja hapo juu imekuwa na
mafanikio makubwa kuongeza maradufu udahili wa wanafunzi katika shule za msingi
na sekondari, kuleta usawa wa kijinsia na kupunguza kwa kiasi kikubwa upungufu
wa walimu, maabara, vitabu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia”.
Kwa mukhtadha huo ni dhahiri kwamba fursa za
Binary
First Lady of Tanzania Scholarship zimekuja kwa wakati muafaka kabisa
ambapo shule zetu za sekondari na taasisi za elimu ya juu zinatoa wahitimu
wengi wanaohitaji kupata elimu za ngazi za juu za shahada za uzamili na uzamivu. Hivyo basi narudia kuwashukuru kwa moyo wenu
wa upendo na ukarimu. Mmeifanyia nchi
yetu ihsani kubwa”, alisema Mama Kikwete.
Naye Mwanzilishi na
Mwenyekiti Mtendaji wa chuo hicho Prof. Joseph Adaikalam alisema nia ya
ufadhili huo wa masomo ni kutoa nafasi kwa wanafunzi watanzania kupata ujuzi na
utaalamu maalum ili watakapomaliza masomo yao na kurudi nyumbani waweze
kuchangia katika maendeleo ya nchi na kuwasaidia moja kwa moja watanzania.
“Binary - First Lady Scholarships ambayo iko chini ya
mwamvuli wa Binary Global Scholarship Fund ilianzishwa mwaka 2009 hadi sasa
nafasi hizo za masomo zimeshatolewa katika nchi za Zambia, Kenya na Senegali”.
Pia chuo kinatoa ufadhili
wa masomo kwa nchi ambazo hazina mke wa Rais ufadhili unaojulikana kwa jina la Binary
Malaysia – Bosnia Herzegovina, na Binary Malaysian - Uzbekistan hii yote ni
kuonyesha kuwa vyuo vikuu vya Malaysia
vinatambua umuhimu wa elimu”, Prof. Adaikalam.
Alisema wanafunzi wataoomba
ufadhili huo wa masomo kwa shahada ya Uzamili kiwango chao cha ufaulu kitaanzia
CGPA ya 3.5 na kuendelea na watakaokidhi vigezo wataanza masomo mwezi wa 10
mwaka huu nchini humo.
Taasisi ya WAMA ni
msimamizi wa Binary - First Lady of Tanzania
Scholarship utakaotolewa kwa kipindi cha miaka mitatu na baada ya hapo
utasainiwa tena kwa kipindi kama hicho na kwa mwaka huu nafasi zitatolewa kwa wanafunzi wa masomo ya Uzamili. Mwakani ufadhili
utatolewa kwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Uzamivu.
No comments:
Post a Comment