Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Tumieni mtandao huu ni wenu nyote.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ameielekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
kuhakikisha kuwa Balozi mbali mbali za Tanzania nje ya nchi zinakuwa na
Waambata wa Elimu kwa nia ya kukabiliana na kutatua matatizo ya
wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika nchi mbali mbali duniani.
Aidha, Rais
Kikwete amesema kuwa moja ya wajibu mkubwa wa mabalozi wanaoziwakilisha
Tanzania nje ya nchi ni kutetea na kulinda maslahi ya Watanzania
walioko katika nchi hizo, bila kujadili kama Watanzania hao wamepelekwa
nje na Serikali ama wamekwenda huko kwa njia nyingine.
Rais
Kikwete amefanunua mambo hayo wakati alipozungumza na viongozi wa
wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya
juu katika Algeria, nchi ambayo Rais Kikwete anaitembelea rasmi kwa siku
tatu kuanzia jana, Jumamosi, Mei 9, 2015. Tanzania ina kiasi cha
wanafunzi 370 katika Algeria kwa sasa.
Rais
Kikwete alizungumza na viongozi hao wanafunzi kwenye siku ya kwanza ya
ziara yake rasmi ya Kiserikali katika Algeria usiku wa jana, Jumamosi,
Mei 9, 2015.
Akizungumza
na viongozi hao wa wanafunzi, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania ina
wanafunzi wengi katika nchi mbali mbali duniani, wanafunzi ambao
wanahitaji huduma mbali mbali za kibalozi na hivyo ni lazima itafutwe
namna ya kurejea katika utaratibu wetu wa zamani wa kuwa na Waambata wa
Elimu katika balozi mbali mbali za Tanzania nchi za nje.
“Ni
lazima tuwe na Waambata wa Elimu kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya
vijana ….wanafunzi wetu nje ya nchi. Kila ninapokwenda nakabiliana na
matatizo kama haya mnayoniuliza nyie na mengine mengi na ya aina mbali
mbali ya wanafunzi,” Rais Kikwete amwaambia wanafunzi hao mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe.
Kuhusu
nafasi ya mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za nje, Rais
Kikwete amesema kuwa ni shughuli muhimu ya kila balozi wa Tanzania
katika nchi mbali mbali kushughulikia matatizo ya Watanzania.
“Mabalozi
wetu kushughulikia matatizo ya Watanzania ni wajibu wao iwe ni wale
Watanzania wanaopelekwa nje na Serikali ama wale ambao kwa njia moja ama
nyingine wamejikuta nje ya nchi hata kama hawakupelekwa na Serikali.
Huu ndio wajibu wa kila balozi wa Tanzania popote alipo,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alianza ziara rasmi ya Kiserikali ya Algeria jana kwa mwaliko wa Rais Abdelaziz Bouteflika.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
10 Mei, 2015
No comments:
Post a Comment