Social Icons

Thursday 8 May 2014

Hatari sana:Wanafunzi watumia mitandao kutafuta wapenzi


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu amewasihi wanafunzi wa kike, kuacha kukimbilia ngono na kutumia mitandao ya kijamii, kutafuta wapenzi wapya kama wanataka kutimiza ndoto zao za kimaisha.
“Wapo wenye ndoto za kuolewa mara tu baada ya kumaliza elimu ya msingi; sijui kimaisha wanajiweka katika kundi gani?” alisema.
Alisema urithi pekee kwa mwanafunzi wa kike ni elimu, ambayo kama utachanganya na ngono unaweza usitimie kwani mbali na mimba, magonjwa ya zinaa na Ukimwi yanaweza kuvuruga matarajio yake.
Aliyasema hayo kwenye mahafali ya 22 ya wanafunzi wa kidato cha sita wa shule ya sekondari ya wasichana Iringa (Iringa Girls), yaliyofanyika shuleni hapo hivi karibuni.
Msambatavangu alisema wanafunzi wa kike wanatakiwa wajiamini, wajitambue na kufahamu wajibu wao ili wajikomboe kifikra na kiuchumi kabla ya kutimiza ndoto za maisha yao.
Msambavangu alisema baadhi ya wanaume wamekuwa wakiwasaka kwa udi na uvumba wasichana wa shule wakiamini kufanya nao ngono ni salama pamoja na uwezekano wa kupata magonjwa ya kujamiiana na mimba.
Alisema utafiti mbalimbali, umeonesha kuwepo kwa kiu kubwa ya kufikia mafanikio ya juu miongoni mwa wanafunzi wa kike lakini kwa baadhi yao kiu hiyo imekuwa ikikatizwa na wanaume wakware.
“Asilimia kubwa ya wazazi wanataka mtoto wa kike asome ili afikie ngazi kubwa kama ilivyo kwa viongozi wa kike walio madarakani lakini kwa tamaa ya fedha na anasa wengi wenu mmekuwa mkiishia njiani,” alisema.
Aidha, alitaka kuacha tabia ya kutumia kwa muda mrefu mitandao ya kijamii kutafuta marafiki wa kiume kwa kubadilibadili picha zenye pozi za kutamanisha.
“Tumieni mitandao hiyo kwa mambo mnayoona yatawaongezea uelewa katika harakati zenu za kutafuta elimu kwa maisha yenu, acheni kutumia mitandao hiyo kwa mambo yasio na msingi,” alisema.
Katika harambee ya kuchangia ununuzi wa gari la shule hiyo, linalokadiriwa kuwa na thamani ya Sh milioni 25, Msambatavangu alichangia Sh milioni 1.5 kati ya Sh milioni 4 .6 zilizopatikana.
Mkuu wa shule hiyo, Joyce Msigwa aliwashukuru wazazi wa wanafunzi kwa michango yao, itakayowezesha shule hiyo kukabiliana na changamoto kubwa ya usafiri. Inapotokea dharura ikiwemo ya ugonjwa, Msigwa alisema wanafunzi wanakabiliwa na wakati mgumu kwasababu ya ukosefu wa usafiri.
“Tunaomba wadau mbalimbali, wazazi na makampuni mbalimbali watuchangie ili tupate gari litakalopunguza changamoto tulizonazo,” alisema.
Habari Leo

No comments: