Na Anna Nkinda – Maelezo , Dodoma
Wanafunzi
wa kike wa vyuo vikuu nchini wametakiwa kujitambua na kufahamu wajibu
wao kwa jamii inayowazunguka kwa kufanya hivyo wataweza kujiepesha na
vishawishi mbalimbali vikiwemo vya ngono na kujikomboa kifikra,
kiutamaduni na kiuchumi na hivyo kutimiza ndoto za maisha yao.
Pia
wametakiwa kujuwa thamani yao na kuepuka kutumiwa vibaya na kushinda
majaribu ya watu wanaotaka kuivuruga safari yao ya maisha na
kutokubali mtu kuwajaza hofu na kuyumbisha uthubutu wao.
Mwito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na
wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu waliohudhuria kongamano la mustakabali
wa mtoto wa kike katika mazingira ya sasa lililofanyika katika ukumbi wa
Chimwaga uliopo chuo kikuu cha Dodoma (UDOM).
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema kila mtu amepewa karama za kumuwezesha kufikia wito wa
kutimiza ndoto zake ili kuweza kufanikisha hayo hana budi kujitambua,
kuvitunza na kuvilea vipawa na karama zake na kuyakubali madhaifu yake
katika kutimiza azma zake.
“Kataa
kabisa mawazo ya kukatisha tamaa kwani hofu kama ilivyo furaha
huuambukiza , jaribu kuwaepuka marafiki wenye mawazo ya kukatisha tamaa
kwani hao ndiyo maadui wakubwa wa maisha yako na wa kukukwamisha kufikia
malengo yako.
Kuna
wakati inawezekana ukawa na hamu ya kuona malengo yako yanatimia mara
moja ukweli ni kwamba hamu yako ya kuleta mabadiliko ya haraka yanaweza
kukuletea madhara makubwa kuliko faida na hapa ndipo mabinti wengi
uharibikiwa kwa sababu wanakosa subira na hivyo kufanya mambo yao
kinyume na utaratibu na malengo”, aliasa Mama Kikwete.
Aidha
Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwahimiza wanafunzi hao kugombea nafasi
mbalimbali za uongozi katika vyuo vyao kwa kufanya hivyo watajiwekea
mazingira mazuri ya kuwa viongozi wa baadaye pindi watakapomaliza masomo
yao kwani viongozi wengi wanaowaona leo walianza kujishughulisha na
uongozi wakiwa wanafunzi.
Mama
Kikwete alisema, “Wanawake tuna nafasi ya pekee ya uongozi kwani sisi
ndio wazazi na walezi tunaokabiliwa na changamoto nyingi, hivyo basi
sisi tuna mchango wa pekee katika kutatua changamoto hizo lakini
tutaweza kufanya hivyo kama tutaingia katika ngazi ya maamuzi jambo la
muhimu ni kupendana na kuungana katika mambo ya maendeleo kwa ajili ya
maslahi yetu kama wanawake”.
Akisoma
Risala ya wanafunzi hao mwakilishi wa wanafunzi Hamida Salum alisema
katika maisha suala la kujitambua ni la muhimu kwakuwa wanafunzi wengi
wa elimu ya juu wanasoma bila ya kuwa na malengo hali hii husababishwa
na kutojitambua kunakowapelekea kupoteza mwelekeo kwani lengo kuu
linalowapeleka vyuoni ni kupata elimu.
Hamida
alisema, “Changamotozinazomkabili mtoto wa kike ni nyingi baadhi ni
kutokuwa na elimu ya afya ya uzazi na jinsia jambo ambalo limesababisha
wasichana wengi kujihusisha katika mahusiano yasiyo salama, dhana
potofu ambayo imejengeka katika jamii kwamba wanawake hawawezi kuwa
viongozi kiasi cha kuwaathiri hata watoto wa kike wenye uwezo wa
kuongoza.
Sera
nyingi za nchi yetu zimemsahau mtoto wa kike katika mambo yanayomuhusu
na hivyo kumfanya aonekane ni mtu duni kwenye jamii kwani tumekuwa
tukishuhudia wazee, watu wazima wakiwarubuni wanafunzi wa kike na kuwa
na mahusiano nao ya kimapenzi ambayo yamepelekea wasichana wengi kupata
ujauzito na hatimaye kufukuzwa shule”.
Wanafunzi
hao pia waliiomba Serikali itazame upya sera ya utoaji wa mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu hasa wasichana kwakuwawengi wao hawakidhi
vigezo vya kupewa mikopo na wanahitaji kusoma hivyo wanafunzi wanaotoka
katika familia zenye uwezo duni kiuchumi kushindwa kuendelea na masomo.
Kwa
upande wake mtoa neno la shukrani Zakiah Mbuma ambaye ni mwakilishi wa
wanafunzi alimshukuru Mama Kikwete kwa kukubali mwaliko wao na kuweza
kushiriki nao katika kongamano hilo ambalo limewasaidia kujifunza mambo
mengi kutokana na nasaha zake pamoja na mada zilizitolewa.
“Hivi
sasa tumeweza kujitambua na kufahamu thamani yetu hapo ndipo tunaweza
kufikia malengo , kutambua mazingira au wakati sahihi wa kufanya jambo ,
kwakuwa kila msichana amepewa vipawa na karama zake jambo la muhimu ni
kukubali madhaifu na kuepuka kutumiwa vibaya”, alisema Zakiah.
Kongamano
hilo la siku moja liliandaliwa na Chuo kikuu cha Dodoma na kuhudhuriwa
na wanafunzi wa kike zaidi ya 3000 kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara
(CBE), Chuo kikuu cha Mt. John, Chuo kikuu Mzumbe, Chuo cha Mipango,
Chuo cha Hombolo, Chuo cha Madini na Shule ya sekondari Dodoma.
Baadhi
ya viongozi wa Serikali na vyama vya siasa wakiwemo mawaziri, wabunge
na wajumbe wa bunge la katiba walihudhuria kongamano hilo ambapo mada
mbalimbali zilitolewa ikiwa ni pamoja na malengo ya kujitambua, uongozi,
afya ya uzazi na ujinsia na nafasi ya mtoto wa kike katika katiba mpya.
No comments:
Post a Comment