Social Icons

Thursday, 20 March 2014

TAARIFA MUHIMU: BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU YAZUNGUMZA NA WANAHABARI DAR ES SALAAM LEO



 Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, elimu na mawasiliano wa bodi ya mikopo Tanzania, Cosmas Mwaisobwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es salaam
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, elimu na mawasiliano wa bodi ya mikopo Tanzania, Cosmas Mwaisobwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es salaam jana kuhusiana na masuala ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini. Pamoja nae ni Ofisa Mwandamizi Habari, elimu na mawasiliano, Veneranda Malima. 
 *********
 1.0     UTANGULIZI

 Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilianzishwa kwa sheria Na. 9 ya mwaka 2004 na kuanza rasmi majukumu yake Julai 2005. Bodi ina majukumu makuu mawili; kwanza ni kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu kwa ajili ya masomo ya Shahada au Stashahada ya juu. 
Jukumu la pili ni kukusanya marejesho ya mikopo iliyotolewa kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu tangu mwaka 1994.

2.0        UTOAJI WA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
 Tangu kuanzishwa kwake, Bodi imefanikiwa kutoa mikopo kwa idadi kubwa ya Wanafunzi ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla Bodi haijaanzishwa. Mwaka 2005/2006 Bodi ilipoanza kazi ilitoa mikopo kwa Wanafunzi 42,729 wa elimu ya juu kwa kutumia bajeti shilingi Bilioni 56.1.

Idadi ya Wanafunzi wa elimu ya juu wanaopewa mikopo imeendelea kuongezeka kutoka  wanafunzi 42,729 mwaka 2005/2006 hadi Wanafunzi 97,348 mwaka 2012/2013. Hii ni sawa na ongezeko la wastani wa 10.4% kwa mwaka. Mikopo iliyotolewa kwa Wanafunzi wahitaji iliongezeka kutoka TZS 56.1 Bilioni mwaka 2005/2006 hadi TZS 306 Bilioni mwaka wa fedha 2012/2013.

Kwa mwaka wa masomo 2013/2014, jumla ya wanafunzi 95,178 wamenufaika na mikopo hadi kufikia tarehe 15 Machi, 2014 ambao mikopo ya kiasi cha TZS 223,977,042,853.00 imekwishalipwa.



Mwaka
Idadi ya Wanafunzi Waliokopeshwa
Ongezeko
(%)
Kiasi kilichoko-peshwa
(Tshs Bilioni)
Ongezeko
(%)
2004/05 (Na Wizara)

16,345

-

9.9

-
2005/2006
42,729
161.4
56.1
467
2006/2007
47,554
11.3
76.1
35.7
2007/2008 
55,687
17.1
110.8
45.6
2008/2009
58,798
5.6
139.0

25.5
2009/2010
72,035
18.4
237.8
28.7
2010/2011
92,791
28.8
230.0
24.5
2011/2012
94,533
2.0
311
35.0
2012/2013
97,348
2.9
335.2
7.2
Wastani wa Ongezeko

30.9

83.7

 3.0     UREJESHAJI WA MIKOPO
 Kuanzia mwaka 1994/1995 hadi tarehe 30 Juni 2013, mikopo yenye jumla ya shilingi 1,502,620,320,764.58 ilitolewa kwa wanafunzi 260,150 ambapo shilingi 51,103,685,914.00 zilitolewa kwa wanafunzi 48,370 na iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kabla ya kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo, na shilingi 1,451,516,634,850.58 kuanzia mwaka 2005/2006 hadi 2012/2013. 

Kati ya shillingi 1,502,620,320,764.58 zilizokopeshwa kwa wanafunzi kati ya mwezi Julai 1994 hadi tarehe 30 Juni, 2013, ni kiasi cha shillingi 512,450,004,489.75 tu ndiyo kimeiva na kuwa tayari kurejeshwa.  Kiasi kingine cha shillingi 990,170,316,274.83 bado hakijaiva kwa sababu wanafunzi walionufaika na mikopo hiyo bado wanaendelea na masomo au wako katika kipindi cha “grace period”. 
Jumla ya mikopo iliyokusanywa hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2014 ni shilingi 45,149,255,508.94 ambazo ni  sawa na asilimia 57% ya “instalments” zilizokuwa tayari kukusanywa (Shillingi 79,510,010,031.18).

Kuanzia mwezi Septemba, 2013, Bodi ilianzisha utaratibu mpya wa kurejesha mikopo kwa njia mtandao.  Sasa warejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu wanaweza kurejesha mikopo yao kupitia huduma ya M-Pesa.  Kuanzia mwezi April, 2014 mikopo pia itaweza kurejeshwa kupitia Airtel Money.

Kabla ya kuanza kutumia huduma ya M-pesa, Mnufaika wa mkopo anapaswa kuwasiliana na Bodi ili kupata taarifa muhimu zifuatazo:-

·         Taarifa ya mkopo (Loan Statement)
·         Kiwango cha marejesho (Loan Instalments)
·         Namba ya  kumbukumbu (Loan Number)

4.0 MAOMBI YA MIKOPO KWA MWAKA WA MASOMO 2014/2015 (KWA NJIA YA MTANDAO)

Bodi ilizindua matumizi ya mtandao katika maombi ya mikopo kuanzia mwaka wa masomo 2011/2012.  Mfumo huu wa maombi ya mikopo umerahisisha sana zoezi la uombaji mikopo na pia umepunguza tatizo la upotevu wa nyaraka.

Maandalizi kwa ajili ya utoaji mikopo kwa mwaka ujao wa masomo yanaendelea.  Maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa mwaka wa masomo 2014/2015 yanatarajiwa kuanza kupokelewa kuanzia mwishoni mwa mwezi Aprili 2014. Katika kipindi hicho, waombaji wa mikopo ya Wanafunzi wa elimu ya juu watapaswa kulipa ada ya maombi (shilingi 30,000) kwa njia ya M-Pesa na kisha kujaza taarifa zao kwa njia ya mtandao. Baada ya kukamilisha maombi kwenye mtandao na kuchapa fomu iliyokamilika, mwombaji atatakiwa kuweka viambatanisho muhimu ikiwa ni pamoja na nakala ya cheti chake cha kuzaliwa,  nakala za vyeti vya taaluma na uthibitisho wa mdhamini wake vikiwa vimeshuhudiwa na Wakili/Hakimu na Mtendaji wa serikali ya mtaa wa mahali mwombaji wa mkopo anapoishi. Nyaraka hizo zitumwe na mwombaji kwa njia ya Posta ili kukamilisha taarifa alizozijaza awali kwa njia ya mtandao.

Kwa kuzingatia mahitaji ya waombaji wa mikopo, Bodi hutoa msaada kwa waombaji wanaokumbana na matatizo madogo madogo wakati wa kujaza fomu. Dawati maalum la msaada kwa wateja limeanzishwa kwa ajili hiyo.  Msaada huu utatolewa kwa njia simu siku ya Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 2 usiku, na siku ya Jumamosi kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa kumi jioni kwa kipindi chote cha maombi ya mikopo.  Hivyo, waombaji wote watakaopata matatizo katika zoezi hilo wanaombwa kutumia dawati hili la msaada kwa wateja.

5.0          CHANGAMOTO

Bodi inakabiliana na changamoto kadhaa ambazo ni pamoja na:
  • Imani potofu iliyoenea kwamba mikopo inayotolewa na Bodi ni ruzuku
  • Ufinyu wa Bajeti kukidhi mahitaji ya waombaji wa mikopo
  • Ushirikiano hafifu na baadhi ya waajiri katika urejeshaji mikopo
  • Kutokuwepo kwa vitambulisho vya Utaifa.

6.0        HITIMISHO

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inaendelea kuwaelimisha wadau wake na umma kwa ujumla juu ya umuhimu wa kuchangia elimu ya juu na kwamba ni muhimu kuzingatia kuwa mikopo hii ni kwa ajili ya wanafunzi wahitaji ili waweze kufikia malengo yao ya kupata elimu ya juu.

Hali kadhalika,  Bodi kwa kutambua jukumu lake la kusimamia urejeshaji wa mikopo inaendelea kuhimiza wanufaika wote wa mikopo kurejesha mikopo hiyo mara tu wanapohitimu masomo yao ili fedha hizo zitumike kusaidia wanafunzi wengine wahitaji wanaojiunga na elimu ya juu.



Imetolewa Na:

Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu

No comments: