Social Icons

Saturday 15 February 2014

CHUO CHA CBE CHAENDELEA KUFANYA VIZURI KIELIMU

CBE - 1
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Janet Mbene (katikati) akiwa ameongozana na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (kulia) mara baada ya kukitembelea chuo hicho jijini Dar es salaam.
CBE - 2
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Janet Mbene akiongea na viongozi wa Chuo cha elimu ya Biashara mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya chuo hicho jijini Dar es salaam.
 CBE - 3
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Janet Mbene akiwa ameambatana na viongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) akiangalia vifaa vya kisasa vya kujifunzia wanafunzi katika chuo wakati wa ziara yake jijini Dar es salaam.
Cbe - 4
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (mwenye suti nyeusi) akimwonesha Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Janet Mbene maeneo ya chuo hicho yaliyovamiwa ambayo sasa yamejengwa majengo ya biashara.
Cbe - 5
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Janet Mbene akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chuo cha elimu ya Biashara mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika chuo hicho jijini Dar es salaam.(Picha na Aron Msigwa – MAELEZO)
-Yaweka Mifumo ya Kisasa ya Kufuatilia Kudhibiti Ukiukwaji Wa Maadili

Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Serikali imesema kuwa Chuo cha  Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Dar es salaam licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali kimeendelea kufanya vizuri katika nyanja ya elimu kwa kuboresha mafunzo yanayotolewa chuoni hapo, kupanua miundombinu na kuweka mifumo ya kisasa ya kufuatilia vitendo vya ukiukaji wa maadili na udanganyifu unaofanywa na wanafunzi wakati wa mitihani.
 Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh.Janet Mbene wakati akizungumza na uongozi wa chuo hicho mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya chuo hicho leo jijini Dar es salaam.
Amesema chuo hicho kwa muda mrefu kimekuwa mstari wa mbele katika kutoa vijana wenye ujuzi ambao wamekuwa msaada kwa jamii na taifa zima na kuongeza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanyika chuoni hapo kwa kukijengea uwezo kifedha kadri bajeti ya serikali itakavyoruhusu.
“Chuo hiki tunakiamini, kikubwa muendelee kuhakikisha mnapokea wanafunzi wenye vigezo ili wanapohitimu waweze kufanya vizuri na wawe mfano, serikali inaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha chuo hiki kinafanikiwa” amesisitiza.
Mh. Mbene amepongeza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na uongozi wa chuo hicho katika kuhakikisha suala na nidhamu na maadili kwa wanafunzi linadumishwa na kuongeza kuwa huo ni mfano wa kuigwa kwa vyuo vingine hapa nchini katika kujenga taifa lenye vijana wenye maadili.
Ametoa wito kwa  wakufunzi wa chuo hicho kutimiza wajibu wao kwa kusimamia elimu na haki na kuwataka kuepuka vitendo vinavyoweza kuwadhalilisha wanafunzi na kuharibu taswira ya chuo hicho.
“Ninapenda kuona mnasimamia viwango vya elimu na maadili na kukomesha tabia na vitendo vyote vinavyoweza kuharibu taswira nzuri ya chuo” amesema.
Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo hicho ikiwemo uhaba wa fedha za maendeleo, ufinyu wa eneo kutokana na kuwepo kwa baadhi ya watu waliovamia na kujenga katika eneo la chuo na ukosefu wa wakufunzi wa kutosha Mh. Mbene ameeleza kuwa serikali imezipokea changamoto hizo na itazifanyia kazi ili chuo hicho kiendelee kutoa elimu bora.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof.Emanuel Mjema amesema kuwa uongozi wake unaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha hali ya elimu ya chuo na kuweka msisitizo katika kulinda na kudumisha maadili kwa wanafunzi wote wanaoingia na kutoka chuoni hapo.
Amesema suala la elimu sasa limepewa kipaumbele ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaohitimu wanakuwa bora na wanakidhi viwango kitaifa na kimataifa na kuongeza kuwa chuo kwa sasa kimefanikiwa kudhibiti kabisa vitendo vya udanganyifu vilivyokuwa vikifanywa na wanafunzi wakati wa mitihani.
“Tangu nimeingia madarakani mwezi Januari 2013 nimefanikiwa kubadilisha utaratibu wa mfumo wa utungaji wa mitihani, mfumo huu haumpi mwanafunzi fursa ya aina yoyote ya kuweza kuibia wakati wa mitihani wala kushirikiana na mwanafunzi, sasa mwanafunzi analazimika kusoma kwa bidii na kila mtu anatimiza majukumu yake ” amesisitiza.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha chuo hicho kinaimarisha maadili kwa wanafunzi na wakufunzi hasa madarasani na wakati wa mitihani tayari kamera 20 za kisasa zimekwifungwa kwenye vyumba vya madarasa 20 na matukio yote hurekodiwa na kuwa ushahidi pale yanapotokea madai ya udanganyifu au kuonewa wakati wa mitihani.
“ Kwa sasa hatuna utani na suala la elimu maana wapo waliokumbwa na adhabu mbalimbali kufuatia kuwepo kwa vifaa hivi ambavyo vimetoa ushahidi mzuri na tayari mwalimu mmoja amekwishafukuzwa kazi kwa kukosa nidhamu na toka 2013 hadi sasa hali iko shwari kabisa” amebainisha Prof. Mjema.
Naye Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho (COBESO) Bw. Benedict Masasi akizungumza wakati wa ziara hiyo amesema kuwa kwa sasa hali ya chuo na masomo inakwenda vizuri, wao kama serikali ya wanafunzi hawana malalamiko kutoka kwa wanafunzi kutokana na uelewa uliojengeka miongoni mwa wanafunzi na kuongeza kuwa wao kama serikali ya wanafunzi wanafanya kazi bega kwa began a uongozi wa chuo.

No comments: