Social Icons

Tuesday 28 January 2014

MAHAFALI YA 7 YA DIT, TAASISI YA TEKNOLOJIA YA DAR ES SALAAM, YAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM


NA: HIDAN .O. RICCO.
 
Mahafali ya saba ya Taasisi ya Teknolojia ya Dar Es Salaam imefanyika wiki iliyopita jijini DSM ikihudhurisha wahitimu zaidi ya 500 katika ngazi ya  Astashahada, Stashahada na Shahada ya juu. 

Taasisi ya Teknologia ya Dar Es Salaam, DIT ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Chuo cha Ufundi cha Dar Es Salaam, maarufu kama Dar Tech, inayo Idara 8 kama ifuatavyo, Idara ya Uhandisi Kompyuta, Idara ya Uhandisi Ujenzi, Idara ya Uhandisi Migodi, Idara ya Uhandisi Umeme, Idara ya Uhandisi Elektroniki na Mawasiliano ya Anga, Idara ya Uhandishi Mitambo, Idara ya Sayansi na Teknologia ya Maabara, Idara ya Teknologia ya Habari. 

Wahitimu kutoka Idara mbalimbali walitunukiwa Vyeti, Diploma, na Shahada ya juu kulingana na masomo waliyochukua. 

Mgeni Rasmi katika Hafla hiyo alikuwa Mheshimiwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbaraw, Mbunge akimuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Gharib Bilal,  ambaye alikuwa na udhuru. 

Maandamano ya mahafali yalianza saa 7.30 mchana kwa Wahitimu kuingia viwanja vya michezo katika Taasisi hiyo, na Mgeni Rasmi aliwasili muda wa saa 8.00 akiongozana na jopo na Wahadhiri pamoja na Mkuu wa Taasisi Profesa John Kondoro. 

Baada ya Mlau [Chief of Protocol] kutoa salamu za makaribisho, na kusimika Rungu rasmi katika meza iliyoandaliwa kama inavyofanya katika ukumbi wa Bunge, Wimbo wa Taifa uliimbwa na baadae Mkuu wa Taasisi alisoma hotuba yake, ikifuatiwa na hotuba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Teknolojia ya Dar Es Salaam ambaye ndie aliyemkaribisha Mgeni Rasmi kusoma hotuba yake na baadaye zoezi la kutunuku Vyeti kuanza.
 
Wahitimu wa ngazi ya cheti [Astashahada] katika fani ya Ufundi wa Teknolojia ya Habari yaani Basic Technician Certificate in Information Technology, ndio waliokuwa wa kwanza kutunukiwa wakifuatiwa na Idara zingine, na hatimaye kumalizia na Wahitimu wa Shahada ya Juu.

Wahitimu 49 wa fani ya Uhandisi Ujenzi, yaani Bachelor of Engineering in Civil Engineering ndio waliokuwa wa kwanza kutunukiwa Shahada ya juu wakifuatiwa na 24  wa fani ya Uhandisi Kompyuta yaani Bachelor of Engineering in Computer Engineering. 

Wahitimu wote wa Shahada ya Juu mara baada ya kutunukiwa Shahada zao walivaa rasmi kofia zao kuashiria kwamba sasa ni wahitimu kamili, huku brass band ya Jeshi la Magereza wakipiga wimbo maalum wa fan fair wakati wahitimu kutoka Idara mbalimbali wakitajwa majina yao na kuinuka katika viti vyao na kujipanga mbele ya Jukwaa la Mgeni Rasmi kupokea tuzo hizo.
 
Zoezi la mwisho lilikuwa ni kutangazwa rasmi kwa Wahitimu bora wa kila Program na Idara wanazotoka. Upande wa Stashahada walikuwa wahitimu 8 wote wa jinsia ya kiume, na upande wa Shahada waliotunukiwa walikuwa wahitimu 5 wanne wakiwa ni wanaume na mmoja ni msichana aliyetambulika kwa jina la Cecylia Kuguru, ambaye alishangiliwa na ukumbi mzima uliokuwa umefurika na wazazi, walezi, wanafunzi pamoja na wageni waalikwa.
 
Mgeni Rasmi Profesa Makame Mbarawa kwa Mamlaka aliyopewa alitangaza hapo hapo kumpa scholarship  ya kusoma Masters Degree mhitimu huyo katika Chuo chochote atakachopenda. 

Tamko hilo liliongeza vifijo na nderembo uwanjani hapo huku Mgeni Rasmi akiwahimiza wanafunzi wengine kusoma kwa bidii, kuwa wanafunzi bora na hatimaye kujipatia nafasi kama hizo za kusomeshwa bure na Serikali.
Mhitimu Cecylia Kuguru anatokea Idara ya Uhandishi Elektroniki na Mawasiliano Anga, mafunzo ambayo yanamuwezesha kupata ajira na nafasi ya Juu katika Idara ya Mawasiliano ya angani kama Control Tower ya Mawasiliano ya ndege, meli na kadhalika. 

Mwanafunzi Mhitimu bora ndugu Elias Eliud kwa niaba ya wahitimu wenzake alitoa neno la shukrani, na baadaye sherehe zilifungwa kwa kupigwa picha za pamoja Wahitimu bora na Mgeni Rasmi, Wakuu wa Idara pamoja na Wageni Waalikwa.
 

No comments: