Social Icons

Monday 27 January 2014

CHUO KIKUU CHA DODOMA CHAZALISHA WATAALAM WA MAFUTA


CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) Juni mwaka huu kitatoa wataalamu wake wa kwanza wa masuala ya mafuta, kikiwa ndio chuo cha kwanza kuzalisha wahandisi wa petroli nchini. Akizungumza na gazeti hili, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof Idrisa Kikula alisema kuwa ufundishaji wa masuala ya petroli utakwenda sambamba na wa masuala ya gesi, kwa kuwa programu hiyo inahusu nishati hizo mbili kwa pamoja.
“Tulianzisha programu hii mwaka 2010 tukiwa wa kwanza kuifundisha hapa Tanzania. Uamuzi wa kuianzisha ulitokana na changamoto tuliyoipata kutokana na kugunduliwa kwa gesi nchini,” alisema Kikula.
Kufuatia maelezo yake, muda wa masomo ya nadharia na vitendo kwa waliojiunga na programu hiyo utakwisha Juni lakini wahusika watatunukiwa shahada zao Novemba mwaka huu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Ardhi cha UDOM, Prof Justine Ntalikwa alisema kuwa programu hiyo ilianza ikiwa na wanafunzi 17 na ndio hao wanaotarajiwa kuhitimu katika kipindi hicho, wakiwa na utaalamu wa kutosha kutoa mchango unaohitajika kwenye sekta ya mafuta na gesi.
Alisema, “Kwa kipindi hiki cha mwanzo tunatoa shahada ya kwanza (digirii) tu na tunazalisha wahandisi wa nishati ya petroli pamoja na wajiolojia wa mafuta.”
Alisema, programu hiyo ni ya miaka minne na inajumuisha wiki nane za mafunzo ya nadharia darasani na wiki 30 za mafunzo kwa vitendo kila mwaka.
“Tunaamini kuendelea kuzalisha wataalamu wa mafuta kutaziba pengo kubwa la watu hao katika siku za usoni,” alisema na kuongeza kuwa uwezo wa wahadhiri wanaofundisha masuala hayo ya mafuta ni wa juu wenye kuweza kutoa wataalamu wa kuaminiwa kuendesha sekta ya mafuta.

Chaanzo : Habari Leo

No comments: