Social Icons

Wednesday 12 December 2012

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MGOGORO WA WAFANYAKAZI NA WANAFUNZI KATIKA CHUO KIKUU KISHIRIKI DAR ES SALAAM CHACHUO KIKUU CHA KIMATAIFA CHA KAMPALA



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 
TUME YA VYUO VIKUU TANZANIA


Kwa takribani wiki tatu sasa kumekuwa na mvutano baina menejimenti kwa upande mmoja na wafanyakazi na wanafunzi kwa upande mwingine wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es salaam ama, kinavyojulikana kwa wengi, KIU. Mvutano huu ulisababisha baadhi ya waalimu kusitisha kufundisha na pia baadhi ya wanafunzi kujikuta katika mgomo hadi mvutano uliojitokeza utakapopatiwa ufumbuzi. 
Mvutano huu hatimaye ulisababisha Tume ya VyuoVikuu Tanzania kuingilia kati katika jitihada za kuupatia ufumbuzi. Mnamo tarehe 14 Novemba 2012 Tume iliunda timu ya wataalamu ambao walikwenda katika Chuo hicho na kufanya kazi kwa siku mbili kabla ya kuuanda ripoti yao. Ripoti ilibainisha maeneo mbalimbali yenye changamoto ambazo budi zipate majibu. 
Ripoti hiyo ilijadiliwa katika kikao cha Kamati ya Tume ya Ithibati na Chuo kupewa maelekezo katika maeneo mbalimbali na pia kutakiwa kuleta majibu katika masuala yaliyoonekana kuwa na uhitaji wa majibu. Maelekezo haya yaliwasilishwa Chuoni kwa barua ya tarehe 4 Desemba 2012 yenye kumbukumbu na TCU/A.40/69/Vol.IV/15 na kutakiwa kuleta majibu Tume kabla ya tarehe 30 Desemba 2012. Kabla majibu hayajawasilishwa mgogoro wa wafanyakazi ulianza na kufuatiwa na mgomo wa wanafunzi na hivyo tarehe 11 Desemba 2012 Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu walikwenda katika Chuo hicho ili kuonana hususan na wanafunzi pamoja na menejimenti. Kimsingi, kikao kilihusisha menejimenti na wanafunzi kwa kuwa suala la wafanyakazi lilikuwa limeshapatiwa muafaka wa jinsi ya kulitatua.
Kufuatia mawasiliano ya awali baina ya menejimenti ya Chuo na viongozi wa wafanyakazi kuhusu mishahara ya wafanyakazi ya mwezi wa Novemba 2012 pande zote zilikubaliana kwamba malipo hayo yawe yamefanyika ifikapo tarehe 14 Desemba 2012. 
Pia Chuo pamoja na waalimu wameafiki kufidia kipindi cha masomo ambacho kilipotea wakati wafanyakazi wanashughulikia mstakabali wa mishahara yao. Kufidia huko kutafanyika kati ya tarehe 7 Januari na 11 Februari 2013 ili kutokuathiri mipango mengine ya kimasomo ambayo tayari ilishapangwa kwa kipindi cha sasa hadi Januari 2013. Makubaliano haya yamewasilishwa TCU kwa barua ya Mkuu wa Chuo ya tarehe 10 Desemba 2012 yenye kumbukumbu Na. KIU/PR/Vol.30/11/12. Tume imeelekeza makubaliano haya yatekelezwe bila kukosa ifikapo tarehe 14 Desemba 2012. Ni matumaini ya Tume kwamba hali hii haitajitokeza tena ili shughuli za ufundishaji katika Chuo hicho ziende kulingana na ratiba ya kila semesta.
Kupata taarifa ya yaliyojiri katika kikao baina na menejimenti, wanafunzi, Katibu Mtendaji wa Tume na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu BOFYA HAPA.

No comments: