ZAIDI ya wanafunzi 30,000 wa vyuo vya elimu ya juu nchini kwa mwaka
mpya wa masomo 2017/18, watanufaika na Sh bilioni 427 kutoka Bodi Mikopo
ya Elimu ya Juu (HESLB), huku wanufaika hao wakiwekwa kwenye mikondo
mitatu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul
–Razaq Badru alisema kwa mwaka huu wanufaika wasiopungua 30,000 watapata
mikopo ya elimu kulingana na fani walizochagua kusoma.
Akifafanua idadi na kiwango cha mkopo kitakachotolewa kwa kila mkondo
kulingana na fani watakazosoma, Badru alisema bodi imepanga mikondo
mitatu ya mikopo. Mkondo wa kwanza unawahusu wanafunzi wa fani za afya,
sayansi ya elimu na hesabu, ambapo kundi hilo litapata asilimia 40 ya
mkopo huo ambao ni sawa na Sh bilioni 170.8.
Badru alisema kundi hilo ndilo litapata mkopo mkubwa kuliko makundi
mengine kutokana na fani hizo kuwa adimu na zina mahitaji makubwa ya
soko nchini hasa kwa kuwapata wataalamu watakaosaidia taifa kwenye sekta
za afya, sayansi na elimu.
Mkondo wa pili umepangwa kupata asilimia 35 ya mkopo wote ambao ni
sawa na Sh bilioni 149.45 na wanafunzi watakaonufaika ni wale wa fani za
uhandisi, kilimo, misitu, sayansi ya ardhi, usafirishaji na fani kama
hizo.
Mkondo wa tatu umepangwa kupata asilimia 25 ya mkopo wote ambao ni
sawa na Sh blioni 106.75 na wanufaika wa mkopo huo ni wanafunzi wote
watakaosoma fani za lugha, sanaa, jamii na fani nyingine kama hizo.
Badru alisema pamoja na bodi kuweka mikondo hiyo, lakini pia suala la
jinsia litazingatiwa ili kuepusha jinsi moja kuwa na idadi kubwa ya
wanufaika wa mikopo hiyo. Katika hatua nyingine kwa mwezi mmoja
uliopita, bodi hiyo imekusanya marejesho ya mkopo ya Sh bilioni 31.1
huku ikiweka mikakati ya mwaka huu ya kukusanya kila mwezi zaidi ya Sh
bilioni 14.
Mtendaji huyo wa HELSB alisema lengo lao ni kuhakikisha wanufaika
wote wanafikiwa na kurejesha madeni yao ili yasaidie wengine kupata
elimu. Alisema mikakati yaliyojiwekea kuanzia mwaka huu ni kukusanya
zaidi ya Sh bilioni 14 kila mwezi na kwamba tangu mwaka huu wa fedha
uanze, kwa mwezi Julai pekee wamekusanya Sh bilioni 31.1 huku sekta ya
umma ikiongoza kwa wanufaika wake kurejesha madeni yao.
“Tunakwenda vizuri na tumejiwekea mikakati ya kuhakikisha madeni ya
mikopo hiyo yanarejeshwa ili yaweze kunufaisha wengine, kwa sekta ya
umma tumefanikiwa kuwafikia asilimia 82 ya wadaiwa wote na sekta binafsi
tumefanikiwa kwa asilimia arobaini,” alisema Badru.
Aliongeza kuwa hivi sasa wameweka nguvu kwenye sekta binafsi, kwa
kuwa imekuwa vigumu kuwafikia wadaiwa wote kutokana na sekta hiyo
waajiriwa wake kuhamahama kila wakati au kuacha kazi.
Akizungumzia mikakati ya kukusanya madeni ya mikopo hiyo, Badru
alisema wapo mbioni kuanzisha kampeni ya ‘’Kurejesha mkopo ni uzalendo
uliotukuka’’, itakayofanywa nchi nzima kuhamasisha wanufaika wa bodi
hiyo kujenga tabia ya kurejesha kwa hiari madeni yao.
Alitaja mkakati mwingine ni bodi hiyo hivi sasa iko kwenye hatua za
awali za mazungumzo na taasisi za fedha nchini ili kuona jinsi ya wao
kununua mikopo hiyo ya wadaiwa kupitia waajiri wao.
Awali operesheni ya utafutaji, ufuatiliaji na ukaguzi wa wadaiwa sugu
wa bodi hiyo mahala pa kazi yaliyoendesha mapema mwaka huu kwa kipindi
cha mwaka mmoja uliopita, ilifanikiwa kwa kukusanya Sh bilioni 116 ikiwa
ni kiwango cha marejesho cha asilimia 46, huku awali walilenga
kukusanya Sh bilioni 76.
Hata hivyo, aliwakumbusha waajiri wote nchini kuhakikisha wanatoa
taarifa za waajiri wanaodaiwa na bodi hiyo na kuhakikisha wanakata
asilimia 15 ya mshahara yao na kuipeleka bodi ili kulipa madeni yao.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment