Na. Thobias Robert –
MAELEZO.
Taasisi ya Kiislam ya the
registered Trustees of Masjid Ridhwaa (RTMR), imedhamiria kuanzisha chuo Kikuu
mahsusi kwaajili ya kuwaandaa vijana wa Kitanzania kujiajiri tofauti na ilivyo
sasa kwa baadhi ya vyuo kuandaa wahitimu wanaotegemea kuajiriwa.
Akizungumza na waandishi wa
Habari Jijini Dar es Salaam Leo, Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa Taasisi hiyo, Alhaj Suleiman Seif Nassor, alisema lengo
na dhumuni la taasisi yake ni kuanzisha Chuo Kikuu kitakachoendana na zama hizi
za kidijitali za kuzalisha wataalam watakaoweza kujiajiri wenyewe kwa kutumia
teknolojia zilizopo.
“Chuo Kikuu tunachotarajia
kuanzisha kitatoa wahitimu ambao wao wenyewe watakuwa wenye kujiajiri na pia
kutoa ajira tangu siku ya kwanza ya kuhitimu shahada zao,” alisema Mwenyekiti huyo.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa mifumo
ya utoaji wa Elimu iliyopo katika Vyuo Vikuu vingi hapa nchini, inamjenga mwanafunzi kuwa
tegemezi wa serikali na mashirika binafsi ili yamuajiri lakini wao kama Taasisi
yenye lengo la kuendana na sera ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya
viwanda wana mpango wa kubadilisha mfumo na mtazamo huo.
“Ili kuendana na sera za awamu
hii, taasisi imetafakari kwa kina pamoja na kufanya tafiti mbalimbali na kubaini kuwa ni lazima tubadili muundo wa
utoaji shahada uliopo sasa wa kuandaa watafuta ajira,na badala yake tuandae
wataalamu watakaojiajiri na kuajiri wenzao.
Shahada zinazotarajiwa kuanzishwa
ili kuendana na halihalisi ya soko la sasa, pamoja na mabadiliko ya kisayansi
na teknolojia nipamoja na BSc. Enterpreneur management, BSc. Agricultural
Bussiness, Freelance Photo Journalism pamoja na Corporate communication.
Aidha kwa upande wa miundombinu Mwenyekiti
huyo ameongeza kuwa tayari walishaanza kujenga jengo la Chuo hicho lenye
ghorofa tano na amewaomba watanzania
wenye kiu ya maendeleo kujitoa kwa hali na mali kuchangia ujenzi, ili kuunga
mkono juhudi za Serikali za kuwakomboa watanzania katika lindi la umaskini.
Wakati huohuo Mwenyekiti huyo wa
taasisi ya RTMR amepongeza juhudi zinazofanywa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli
katika kupambana na ubadhirifu wa mali za uuma pamoja na kuleta uwazi na uwajibikaji
katika utumishi wa umma.
“Mh.Rais ameonyesha dhamira ya
dhati kupambana na madawa ya kulevya ambayo yameathiri vijana wengi ambao ni
nguvu kazi ya taifa, hivyo nasisitiza sisi kama viongozi wa dini na watanzania
wote kwa ujumla tumuombee dua ili aweze kukamilisha ndoto yake ya kuifanya
Tanzania kuwa nchi yenye neema “
Alisema.
Miongoni mwa shughuli za
kimaendeleo zinazofanywa na taasisi ya RTMR ni pamoja na Kujenga misikiti,
Vituo vya Afya, Vituo vya Elimu, pamoja na miradi ya kujikwamua kiuchumi kwa
kuzingatia misingi ya kiislam.
Mwisho
No comments:
Post a Comment