Na: Lilian Lundo – MAELEZO - Dodoma
Vyuo Vikuu hapa Nchini vimeagizwa kuacha mara moja kutoza ada kwa fedha za kigeni kwa wanafunzi ambao ni watanzania.
Agizo
hilo limetolewa leo Bungeni, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya alipokuwa akijibu swali
lililoulizwa na Mbunge Jaku Hashimu Ayoub kwamba kumekuwa na malalamiko
ya wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania ambao ni wazawa kulipishwa ada ya
masomo yao kwa fedha za kigeni badala ya fedha za Kitanzania.
“Sarafu
inayotakiwa kutumika Tanzania ni shilingi ya Kitanzania kwa mujibu wa
kifungu cha 25 na 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ya mwaka
2006. Aidha, kwa Tanzania malipo ya kitu au huduma yoyote inapaswa
kulipwa kwa shilingi ya Kitanzania kama ilivyoainishwa kwenye kifungu
cha 28 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, 2006,” alifafanua Mhandisi
Manyanya.
Aliendelea
kwa kusema kuwa japo Wizara haijapokea malalamiko yoyote ya kutozwa
fedha za kigeni kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu tangu itoe agizo kama hilo
kwa wamiliki wa vyuo Septemba 07, 2016.
Hivyo
basi kwa mara nyingine Mhandisi Manyanya ameviagiza vyuo ambavyo bado
vinatoza wanafunzi Watanzania fedha za kigeni kuacha mara moja kwani
vyuo hivyo vimeelekezwa kutoza wananchi wa Kitanzania kwa pesa ya
Kitanzania.
Aidha Mhandisi Manyanya amewataka
watanzania kutoa taarifa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwa
kuna Chuo chochote kinachotoza ada kwa Watanzania kwa fedha za Kigeni
ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Mwisho
No comments:
Post a Comment