Waziri
wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof Jumanne Maghembe akijibu hoja
mbalimbali za wabunge katika kikao cha tisa cha mkutano wa tano wa Bunge
la 11linaloendelea Mjini Dodoma Novemba 10, 2016.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Serikali
imejipanga kuboresha miundo mbinu ya Chuo cha Misitu cha Olmotonyi
kilichopo katika Jimbo la Chambani Mkoa wa Kusini Pemba ili kuwavutia
wanafunzi kujiunga na chuo hicho hivyo kuongeza idadi ya wataalamu wa
misitu nchini.
Hayo
yamesemwa leo mjini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Prof.
Jumanne Maghembe alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chambani Mhe.
Yussuf Hussein lililohoji juu ya mpango wa Serikali kukiboresha chuo
hicho.
Prof.
Maghembe amesema kuwa wameamua kuboresha miundo mbinu ya chuo hicho kwa
sababu kumekuwa na upungufu mkubwa wa wataalamu wa misitu nchini ambapo
kwa sasa kila mtaalamu wa misitu anasimamia jumla ya hekta 25,000 za
misitu kinyume na uwiano unaokubalika kimataifa wa mtaalamu mmoja
kusimamia hekta 5000.
”Serikali
yetu kwa kushirikiana na Serikali ya Norway inaendelea kutekeleza mradi
wa Kuwezesha Jamii kupitia Mafunzo ya Shughuli za Usimamizi Shirikishi
wa Misitu pamoja na Mabadiliko ya Tabianchi, mradi ambao tuna uhakika
utakijengea chuo uwezo na kukiboresha zaidi”, alisema Mhe. Maghembe.
Mhe.
Maghembe ameyataja malengo ya mradi huo kuwa ni kukarabati nyumba saba
za watumishi, kuimarisha maktaba ya chuo kwa kuweka samani, vitabu 137
vya mada 22 tofauti, kuweka vifaa 62 vya kufundishia, kompyuta 15 na
kutoa mafunzo ya kompyuta kwa wakutubi watano, ukarabati wa mtandao wa
mawasiliano pamoja na kuunganisha Chuo na mkongo wa Mawasiliano wa
Taifa.
Mhe.
Prof Maghembe ameongeza kuwa mradi huo unaendelea na ujenzi wa bweni
moja lenye uwezo wa kuchukua wanachuo 100 na ukumbi wa mihadhara wenye
uwezo wa kuchukua wanachuo 200 kwa wakati mmoja.
Aidha,
mradi huu utawajengea uwezo wa mbinu bora za kufundishia wakufunzi 16
na kutoa mafunzo kwa jamii za vijijini kuhusu kuhifadhi misitu na
shughuli mbadala za kiuchumi.
Mhe. Maghembe amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitatu kutoka mwaka 2013 hadi 2016
Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania imegharamia
ukarabati wa nyumba 9 za watumishi, kumbi za chakula kugharamia mikutano
na ununuzi wa kompyuta mbili na gari aina ya Tata kwa ajili ya usafiri
kwa mafunzo ya vitendo nje ya Chuo pia kupitia mradi huo Serikali inatoa
ufadhili kwa wanafunzi wa ngazi ya Astashahada na Stashahada.
No comments:
Post a Comment