MWANAFUNZI wa mwaka wa kwanza Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo
Kikuu cha Dodoma (Udom) Fredrick Joseph (25), ameuawa kwa kushambuliwa
kwa kipigo na watu wanaosadikiwa kuwa ni wanafunzi wenzake.
Tukio hilo ni la juzi usiku katika eneo la chuo hicho, ambapo
mwanafunzi huyo alisikika akipiga kelele, ndipo walinzi wakafika na
kumkuta akiwa anagalagala njiani.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro
Mambosasa, alisema mwanafunzi huyo alishambuliwa kwa kupigwa sehemu
mbalimbali za mwili wake na watu wasiofahamika.
Alibainisha kuwa mwanafunzi huyo alikutwa majira ya saa 10 alfajiri
katika eneo hilo la chuo. Hata hivyo, alisema uchunguzi wa awali
umebaini kuwa mwanafunzi huyo alikuwa na ugomvi na watu hao katika klabu
ya pombe ya Canival Pub iliyopo chuoni hapo.
“Alipoondoka kurudi bwenini akiwa njiani alishambuliwa na watu hao
wasiofahamika na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake, kipigo
kilichosababisha kifo chake wakati alipokimbizwa kutibiwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Dodoma,” alisema Mambosasa.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali hiyo kwa
uchunguzi zaidi na hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na
tukio hilo. Kamanda huyo alisema ameelekeza uchunguzi wa kina ufanyike
kuhusiana na ugomvi huo ili kubaini wahusika.
Wakati huo huo, mkazi wa Kondoa, Amlan Mabata (54) anadaiwa
kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila juzi saa 12 asubuhi kwenye mti
jirani na Gereza Kuu la Isanga Dodoma.
Alisema chanzo cha kujinyonga ni ugomvi wa kifamilia kati yake na
hawara yake, ambaye ni askari magereza wa gereza hilo. Kamanda Mambosasa
alisema Jeshi la Polisi linamhoji askari huyo.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment