Social Icons

Monday 11 July 2016

WAKUU WA VYUO VYA MAENDELEO YA JAMII WATAKIWA KUZINGATIA WELEDI ILI KUZALISHA WATAALAM WENYE SIFA.

Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255629914471. insta : @matukionawanavyuo Tumieni mtandao huu ni wenu nyote.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Erasimus Rugarabamu wakati akifungua kikao kazi cha wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi.Sihaba Nkinga mjini Dodoma.
Baadhi ya Wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa Kikao kazi chao mjini Dodoma leo.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Erasimus Rugarabamu (katikati) akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii wa Wizara hiyo Bw. Enterberth Nyoni (wa pili kushoto) na Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Paschal Joseph Mahinyila wakifuatilia michango mbalimbali ya wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao kazi cha wakuu hao leo mjini Dodoma.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo akichangia jambo

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Erasimus Rugarabamu (katikati mstari wa
mbele) akiwa katika picha ya pamoja na wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii
nchini mjini Dodoma mara baada ya kufungua kikao kazi cha wakuu hao kwa
niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi.Sihaba Nkinga.


Na. Aron Msigwa - Dodoma.
Serikali imewataka Wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini kufanya kazi kwa kuzingatia weledi , kanuni, miongozo na taratibu zinazosimamia uendeshaji wa vyuo hivyo ili kuiwezesha sekta hiyo kupiga hatua kwa kuzalisha wataalam wenye sifa wanaokidhi matarajio ya wananchi.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Erasimus Rugarabamu wakati akifungua kikao kazi cha wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi.Sihaba Nkinga.

Bw. Rugarabamu amewataka wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kuendelea kusimamia kwa umakini mkubwa wa Rasilimali za vyuo hivyo na kubainisha kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa mkuu wa Chuo yeyote atakayeshindwa kuzingatia weledi , sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uendeshaji wa vyuo hivyo.

" Ninyi ndio wasimamizi wa uzalishaji wa wataalam wa Maendeleo ya Jamii nchini, mnao wajibu wa kubadilisha fikra za wananchi na kuwa chachu ya maendeleo, hakikisheni mnasimamia vizuri suala la udahili wa wanafunzi kwa kuwa na wanafunzi wenye sifa.

Aidha, amewataka wakuu hao wa vyuo kuhakikisha kuwa wanapiga vita kwa vitendo udahili wa vyeti vya kughushi ( vyeti feki) akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu kwa Mkuu wa Chuo yeyoye atakayehusika kwa namna moja au nyingine kusaidia udahili wa wananfunzi wasio na sifa.

Ametoa wito kwa wakuu na Wakuu wa taaluma wa vyuo hivyo kuwa makini katika suala la udahili wa wanafunzi wanaojiunga katika fani ya maendeleo ya jamii ili kuendelea kujenga heshima ya taaluma ya Maendeleo ya Jamii na kutimiza matarajio ya kuwaletea maendeleo wananchi.

" Hakikisheni mnaepuka maslahi binafsi katika usimamizi wa taaluma, suala la vyeti feki lisiwe na nafasi katika vyuo vyetu, fanyeni kazi kwa kuzingatia sheria ili tuendelee kutoa wahitimu bora" Amesisitiza Rugarabamu.

Katika hatua nyingine amewataka wakuu hao kuwa wabunifu ili vyuo wanavyovisimamia viweze kuhimili soko la ushindani kutoka vyuo vingine vya elimu ya Maendeleo ya jamiii hapa nchini ili vyuo chini ya wizara, viweze kutekeleza majukumu kwa ufanisi na kuzalisha wataalam wanaokidhi mahitaji ya soko.

" Ili vyuo vyetu viendelee kuonekana lazima viweze kuhimili ushindani kutoka katika vyuo vingine vinavyotoa taaluma kama hii, jambo hili lazima tulifanye kwa nguvu ili tuendelee kuwa wazalishaji bora wa wataalam wa elimu ya Maendeleo ya Jamii hapa nchini" Amesisitiza Rugarabamu.

Aidha, ametoa wito kwa wakuu hao kusimamia vizuri rasilimali za fedha na kufafanua kuwa suala la upimaji wa Wazi wa watumishi wa Umma (OPRAS) lazima lizingatiwe na watumishi wote wa vyuo hivyo kwa kuwa wao ni watumishi wa umma lazima wapimwe utendaji kazi wao kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa.

Aidha, amewataka Wakuu hao kuhakikisha kuwa wanavisimamia vyuo wanavyoviongoza kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha kuwa wanawasilisha taarifa kuhusu maendeleo ya vyuo vyao kwa lengo la kuiwezesha Serikali kuchukua hatua za katika maeneo ambayo hayaendi vizuri kuviwezesha vyuo hivyo kupiga hatua kitaaluma.

Awali akizungumza kabla ya ufunguzi wa mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii wa Wizara hiyo Bw. Enterberth Nyoni amesema kuwa Mkutano huo ni muhimu sana kwa kuwa umewakutanisha wakuu wa Vyuo na Makamu Wakuu wa Vyuo wanaozalisha Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini ambao huajiliwa na Serikali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, taasisi na Mashirika mbalimbali.

Amesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo kuna umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi kupitia mchango wa maafisa maendeleo ya jamii ambao husimamia shughuli za maendeleo ya wananchi kuanzia ngazi ya kijiji, kata hadi Taifa pia usimamizi na utoaji wa elimu kuhusu Haki za makundi mbalimbali katika jamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Paschal Joseph Mahinyila amesema kuwa vyuo vya Maendeleo ya Jamii vinaendelea kufanya kazi nzuri ya kuzalisha wataalam wa masuala ya maendeleo ambao wamekua msaada kwa wananchi.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kuifanyia kazi changamoto ya uhaba na uchakavu wa majengo inayovikabili baadhi ya vyuo vya maendeleo ya Jamii ili viweze kudahili wanafunzi wengi zaidi na kuendelea kutoa elimu katika mazingira bora.

Aidha, amesema kuwa kupitia kikao kazi hicho changamoto ya Miongozo ya uendeshaji itaweza kufanyiwa kazi ili vyuo vyote viweze kuzungumza lugha moja na kutekeleza matakwa ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) pamoja na kuviwezesha vyuo vya maendeleo ya jamii vilivyo chini ya wizara hiyo kuanza kutoa wahitimu wa shahada ya kwanza kwa kujiunga na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Arusha.

Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rugemba, Mafinga mkoani Iringa Bi. Santina Mbata akizungumzia mara baada ya ufunguzi wa kikao kazi hicho amesema kuwa kukutana kwa wakuu hao wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii ni fursa pekee inayowapa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya kisera, kisheria, taratibu na miongozo mbalimbali inayosimamia vyuo hivyo.

Bi.Santina ameeleza kuwa licha ya chuo anachokiongoza kukabiliwa na changamoto mbalimbali Serikali inaendelea kukijengea uwezo ili kuhakikisha kuwa kinaendelea kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake kwa kuendelea kuwajengea uwezo wananchi wanaopata mafunzo kukabilina na changamoto mbalimbali za maendeleo ya wananchi.


No comments: