Social Icons

Thursday 21 July 2016

Vyuo vikuu vyatakiwa kuunga mkono Serikali katika kujenga Tanzania ya Viwanda

Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255629914471. insta : @matukionawanavyuo Tumieni mtandao huu ni wenu nyote. 

Na: Lilian Lundo - MAELEZO

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako  amevitaka vyuo vikuu Tanzania kuunga mkono serikali ya Awamu ya Tano juu ya uanzishwaji wa viwanda kuelekea uchumi wa kati.

Prof. Ndalichako ameyasema hayo leo katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua maonyesho ya kumi na moja ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yatakayofanyika kwa siku tatu kuanzia leo Julai 20 mpaka Julai 22 mwaka huu.

“Vyuo vikuu vinatakiwa kuangalia sera za nchi na mwelekeo wa Taifa kuelekea kukuza uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha wanatoa wataalamu ambao watashiriki katika uchumi wa viwanda ambavyo vitaanzishwa nchini,” alifafanua Prof. Ndalichako

Prof. Ndalichako aliendelea kwa kusema kuwa Serikali iko katika mkakati wa kuboresha vyuo vya ufundi kwa kuanzia na vyuo vitatu vya ufundi vya Dar es Salaam, Arusha na Mbeya ili kuboresha mafunzo wanayoyatoa kuendana na uhitaji uliopo katika uanzishwaji wa viwanda.

Mbali na hayo, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi inashirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika uanzishwaji wa mafunzo katika sekta adimu ikiwemo gesi kwa ajili ya kupata wataalamu watakaoajiriwa katika viwanda vitakavyo anzishwa.

Vile vile wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu hupewa maelekezo ya namna ya kuomba vyuo kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) pamoja na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) katika maonyesho hayo.

Maonyesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia hufanyika kila mwaka yakiwa na Lengo la kutoa elimu kwa wazazi na wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu hapa nchi waweze kujua kozi zinazotolewa katika vyuo hivyo pamoja na maelezo ya kozi hizo

No comments: