Na FATMA SALUM -MAELEZO
Jumla
ya wadaiwa wapya 21,721 wa mikopo ya elimu ya juu wamejitokeza ili
kuanza kulipa madeni yao kufuatia agizo la siku 60 lililotolewa na Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) mnamo Machi 14 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. Robert Kibona wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu tathmini ya agizo lililotolewa na bodi hiyo kwa wanufaika wa mikopo na waajiri ili kutimiza wajibu wao kisheria.
Bw.
Kibona alifafanua kuwa jumla ya Shilingi bilioni 151.5 zinatarajiwa
kurejeshwa na wadaiwa hao ambao walikopeshwa ili kuwawezesha kupata
elimu yao ya juu katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi kuanzia
mwaka 1994.
“Lengo
la agizo lilikuwa ni kuhahakisha madeni yote yaliyoiva yanakusanywa ili
kuongeza uwezo wa kukopesha watanzania wengi zaidi na agizo hili
limeisha Mei 13 mwaka huu.” alisema Bw. Kibona
Kwa
mujibu wa Bw. Kibona, kati ya wadaiwa waliopatikana, wadaiwa 19,528
walipatikana baada ya Bodi kuchambua taarifa za waajiriwa
zilizowasilishwa na waajiiri na wadaiwa wengine wapatao 2,007
walijitokeza kwa hiari.
“Waajiri
wana wajibu wa kisheria wa kuwasilisha taarifa za waajiriwa wao, baadhi
yao walifanya hivyo katika siku hizo sitini na tukawabaini wadaiwa hao,
tunawapongeza waajiri kwa ushirikiano walioutoa na wanufaika wote
waliojitokeza kwa hiari” alisema Bw. Kibona.
Aidha
Bw. Kibona aliongeza kuwa Bodi imeongeza siku 30 za ziada kuanzia Mei
20, 2016 kwa wadaiwa waliobaki kujitokeza na uamuzi huo umetokana na
tathmini iliyoonyesha kuwa kuna idadi kubwa ya waajiri na wanufaika
wanaoendelea kujitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo Bw. Cosmas
Mwaisobwa alisema kuwa kiwango cha ukusanyaji wa madeni kwa mwezi
kinatarajiwa kuongezeka kutoka shilingi bilioni 2.7 zinazokusanywa hivi
sasa na kufikia shilingi bilioni 8 ifikapo mwezi Juni 2016.
Katika
kipindi cha mwaka 1994/1995 hadi sasa, kiasi cha shilingi trilioni 2.44
kimetolewa kwa wanufaika 378,504 wakiwemo wanafunzi wanaoendelea na
masomo yao hivi sasa ambao kwa sasa hawana wajibu wa kulipa hadi pale
watakapomaliza au kusitisha masomo yao.
No comments:
Post a Comment