Social Icons

Friday 22 January 2016

Vyama vya siasa hutumia fedha za walipa kodi.-Kongamano

Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Tumieni mtandao huu ni wenu nyote. 

Chuo kikuu cha Dar es salaam kimefanya kongamano la saba la jumuiya ya wahitimu ambapo mada kuu ilikuwa ''ni tafakuri juu ya uchaguzi mkuu wa 2015'' kwa kuangalia uzoefu,mapungufu,mafunzo na majaaliwa ya baadaye.

Wakichangia katika kongamano hilo Jaji mstaafu Joseph Warioba amesema uchaguzi wa mwaka 2015 ulikuwa ni uchaguzi wa kihistoria ambao ulikuwa na msisimko wa kuanzia kwenye uteuzi wa wagombea pamoja na uendeshaji wa kampeni zake.

Akiichambua mada hiyo Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dkt. Alexander Makulilo amesema kwamba vyama vya siasa hapa nchini bado vina mkwamo wa namna ya kujiendesha na kujipatia mapato na vyote kwa asilimia kubwa vinategemea ruzuku ya serikali.

''Siku ukitoa hiyo ruzuku vyama vitapotea kabisa vyama vinategemea vyanzo vya mapato kwa kutumia kodi za wananchi CCM wanapata asilimia 70%,CHADEMA 17% na vingine hupata chini zaidi ya hapo''

Kwa upande wake Mhadhiri kutoka Chuo kikuu cha Dar es salaam Dkt. Lupa Ramadhani amesema kuwa fedha nyingi sana hutumika kipindi cha uchaguzi na hakuna anaejua fedha hizo zimetoka wapi jambo ambalo linasababishwa na mianya ya sheria,na wakati huo huo vyama vingine vilikosa fedha za kuzunguka na kufanya kampeni.

Akichangia kuhusu mchango wa vyombo vya habari  Dkt. Ayoub Ryoba amesema kuwa vyombo vya habari  vimefanya vizuri zaidi kuliko tulikotoka 1995, kwa kufuatilia kwa ukaribu tume ya uchaguzi,elimu ya mpiga kura pamoja na kuwahabarisha wananchi matukio ya wagombea na jukwaa kwa ajili ya wananchi.

Hata hivyo kwa upande wake mwenyekiti wa kongamano hilo Profesa Issa Shivji amesema kuna umuhimu mkubwa kuangalia kwa undani zaidi suala la kuhoji mahakamani ushindi wa urais kwa ambaye hataridhika na matokeo.

Kongamano hilo limekutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wahadhiri wa elimu ya juu,wanafunzi,vyombo vya habari asasi za kijamii pamoja na wananchi.

 

No comments: