Mbeya. Watu watatu wamefariki dunia wakiwamo wanafunzi wawili wa
Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Mbeya, ambao walipoteza maisha baada
ya kuzama kwenye bwawa la samaki.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi
alisema jana kwamba wanafunzi Michael Tarimo (20) na Albert Shenkalwa
(23) walifariki dunia juzi baada mtumbwi waliokuwa wakiutumia kupinduka
kwenye bwawa maalumu la samaki linalosimamiwa na Hospitali Teule ya
Ifisi eneo la Mbalizi jijini hapa.
Msangi alisema bwawa hilo ni sehemu ya ‘Zoo ya
wanyama’ inayosimamiwa na hospitali hiyo ambapo watu mbalimbali
wanafanya utalii kutembelea na kujionea wanyama wa aina mbalimbali
pamoja na kupanda mtumbwi kwenye bwawa dogo.
Alisema wanafunzi hao walikuwa wakisomea
stashahada ya biashara na kwamba walikwenda huko pamoja na wenzao 12,
kwenye ‘pikiniki.’ Alisema pamoja na kuangalia wanyama pia walikwenda
kwenye bwawa linalotunza samaki ambako walipanda mtumbwi lakini
ulijigeuza ghafla na walishindwa kuogelea.
“Kwa kawaida katika bwawa hilo, watu hawaruhusiwa
kuogelea isipokuwa kuingia kwa mtumbwi,’’ alisema. Kuhusu kifo cha mtu
wa tatu, Kamanda Msangi alisema mkazi wa Kijiji cha Mpolo-Igawa,
wilayani Mbarali Anaheri Lazaro (43) aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa
kwenye kilabu cha pombe za kienyeji. Msangi alisema uchunguzi wa polisi
uligundua kwamba silaha iliyotumika ni gobori baada ya kuokotwa golori
moja eneo la tukio.
Alisema chanzo cha mauaji kinachunguzwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa Kituo cha Afya Igurusi.
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment