Kamishna Msaidizi
wa Madini Mhandisi Hamis Komba katikati
akiwa pamoja na Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma masomo ya Geomolojia katika
Chuo cha ‘Asian Institute of Geological Science’ (AIGS) nchini Thailand. Wa
kwanza kulia ni Agatha Mwinuka, anayefuata ni Emmanuel Minja na wa kwanza
kushoto ni Doricas Moshi.
Wanafunzi wa
Kitanzania nchini Thailand, wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wenzao
kutoka mataifa mbalimbali , ambao wamelitembelea banda la Tanzania.
Wafanyakazi wa
Wizara ya Nishati na Madini katika picha ya pamoja na wanafunzi hao katika
banda la Tanzania.
*************
Wanafunzi wa Tanzania Thailand Waizungumzia sekta ya
Madini.
Na Asteria Muhozya, Bangkok
Wanafunzi wa
Kitanzania wanaosoma masomo ya Geomolojia katika Chuo cha ‘Asian Institute of
Geological Science’ (AIGS) nchini Thailand, wamewataka wadau wa tasnia ya madini
ya vito na usonara nchini Tanzania kuichukua sekta hiyo kwa umakini mkubwa
kutokana na mchango wake kiuchumi.
Aidha, wameeleza
kuwa, nchi ya Thailand imepiga hatua kubwa katika sekta ya madini ukilinganisha
na Tanzania lakini bado Tanzania inaweza kufaidika zaidi katika sekta hiyo ikiwa
kila mdau atatimiza wajibu wake kikamilifu ili madini ya vito yaongeze mchango
katika pato la taifa.
Wameongeza kuwa,
Tanzania bado ina nafasi ya kujipanga upya kuhusu kuboresha zaidi sekta hiyo
kama ilivyo kwa nchi nyingine endapo
mipango mikakati ya maboresho itatekelezwa na kusimamiwa kikamilifu.
Wanafunzi hao wameyasema
hayo, wakati walipolitembelea banda la Tanzania katika maonesho ya 53 ya Vito
vya Usonara na Madini yanayoendelea katika jiji la Bangkok ambapo nchi zaidi ya
150 zinashiriki maonesho hayo.
“Thailand
wamejipanga vizuri katika sekta ya madini. Wafanyabiashara wa madini wana
umoja. Wadau wa madini wanatakiwa kuelewa kuwa madini yanawakilisha utajiri wetu
tulionao”. Amesema Agatha Mwinuka.
Aidha, wameitaka
serikali na wadau wa Tanzania wanaoshiriki maonesho hayo kujifunza kutokana
na changamoto wanazozipata kutoka kwa nchi nyingine, jambo ambalo litasaidia
kuboresha sekta ya madini na vito, ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara
kuhakikisha kuwa wanafuata sheria na
taratibu zilizopo.
“Tunaiomba
serikali iendelee kuendeleza viwanda vya kukata madini. Ni jambo zuri kama
shughuli hizi za kukata madini zitafanyika ndani ya nchi badala ya nje. Jambo
hili linasaidia sana kuongeza thamani ya madini. Ameongeza, Emmanuel Minja.
Akiongelea
kuhusu
umuhimu wa kuendeleza na kuboresha kituo cha Tanzania Geomological
Center, Doricas Moshi, ameeleza kuwa, kituo hicho kinaweza kutoa
mchango mkubwa
katika tasnia hii hasa katika nyanja ya ukataji madini na uthamini wa
madini hivyo, ameitaka
Serikali kukiongezea nguvu kituo hicho kutokana na umuhimu wake kwa
maendeleo
ya Tanzania.
“Chuotunachosoma
hapa kinatumia sana mifano ya madini ya Tanzania katika kufundisha. Mengi yametoka nyumbani, hii ni ishara nzuri. Serikali
iliangalie hili. Ameongeza Doricas.
Aidha, wameeleza
kuwa, soko la kimataifa kwa madini ya Tanzania lipo, hivyo, wamewataka wadau
wote kuhakikisha wanashirikiana vizuri na serikali kuendeleza sekta hiyo
kutokana na umuhimu na mchango wake kwa taifa.
Akizungumzia mipango iliyopo ya kuboresha sekta hiyo,
Kamishna Msaidizi wa Madini, Mhandisi Hamis Komba, amesema kuwa, Serikali
kupitia Shirika la Madini Tanzania (STAMICO), inatekeleza mikakati ya
kuwasaidia wachimbaji wadogo na wa kati ili waweze kuendana na mahitaji ya soko la kimataifa kwa kuwapatia
mafunzo mbalimbali yakiwemo ya kukata madini, kuyaongezea thamani na kuwapatia mikopo kupitia Benki ya TIB.
“STAMICO imepewa
jukumu la kuwaendeleza wachimbaji wadogo katika sekta ya madini hususani katika
masuala ya uchimbaji, uongezaji thamani madini na biashara ya madini. Serikali
imejipanga vizuri katika hilo”. Ameongeza Kamishana.
Ameongeza kuwa,
Serikali inatambua kwamba wachimbaji wengi wapo katika sekta ya madini ya vito
na usonara hivyo, jitihada za kuwaendeleza
zitasaidia kufikia kiwango bora cha utendaji wao wa kazi.
Vilevile,
ameongeza kuwa, kutokana na kuboreshwa kwa Sheria ya madini ya mwaka 2010
ambayo inaiwezesha STAMICO kumiliki asilimia 50 ya hisa katika mgodi wa
Tanzanite One, jambo ambalo linaifanya Serikali kuwa mmiliki katika mgodi huo.
No comments:
Post a Comment