Social Icons

Friday 21 February 2014

SOMA KWA MAKINI: UFAFANUZI KUHUSU HABARI ZILIZOCHAPISHWA KWA LENGO LA KUUPOTOSHA UMMA KUHUSU CHUO CHA CBE


Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Mjema akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu habari za upotoshaji zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku na baadhi ya mitandao ya kijamii kuhusu chuo hicho, leo jijini Dar es salaam.
*******************SOMA KWA MAKINI: UFAFANUZI KUHUSU HABARI ZILIZOCHAPISHWA KWA LENGO LA KUUPOTOSHA UMMA KUHUSU CHUO CHA CBE*****************************
Aron Msigwa – MAELEZO.
Mkuu wa chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema amesema kuwa  habari zilizoandikwa na kuchapishwa na gazeti moja la kila siku na baadhi ya mitandao ya kijamii hapa nchini zililenga kukidhalilisha chuo na kuipotosha jamii kufuatia chuo hicho kuendelea kufanya vizuri katika kulinda maadili na viwango vya taaluma hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam mkuu wa chuo hicho amesema kuwa habari zilizochapishwa kuhusu kuwekwa kwa mfumo wa kamera za kisasa  madarasani na taarifa ya kufukuzwa kwa mwalimu mmoja wa chuo hicho akihusishwa na vitendo vya ngono na wanafunzi zimepotoshwa na vyombo hivyo  kwa  kukosa weledi wa kushindwa kupata uhalisia na usahihi wa habari husika kutoka mamlaka za chuo hicho.
Prof. Mjema amesema kuwa Chuo cha Elimu ya Biashara ni Chuo cha Serikali ambacho kimekua kikitoa  Elimu ya Biashara kwa miaka 49  na kuongeza kuwa chuo hicho kinaajiri wakufunzi wake kupitia utaratibu wa serikali wa kutangaza nafasi za kazi kupitia Tume ya Ajira iliyopo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma.
Ameongeza kuwa chuo hicho kina wakufunzi na wataalam wanaoheshimu maadili ya utumishi wa umma na taaluma zao na kuongeza kuwa chuo hicho kina wakufunzi wenye sifa ambao hawahitaji kufuatiliwa na mtu katika kazi zao.
“Nachopenda kusema ni kwamba chuo chetu sasa kinao wataalam na wakufunzi wenye sifa na walioajiriwa kwa kuzingatia kanuni na vigezo vilivyowekwa,taarifa zilizotolewa hazina ukweli wowote na zimelenga kukidhalilisha chuo na kuipotosha jamii”
Amesema kuwa kamera za  kisasa ziilizofungwa katika vyumba vya madarasa vya chuo hicho zimewekwa kwa lengo la kudhibiti udanganyifu katika mitihani na kuimarisha ulinzi na usalama wa mali za chuo na kuongeza kuwa juhudi zinafanyika katika mwaka ujao wa fedha kuongeza vifaa hivyo hasa katika maeneo ya kuingilia nay ale yanayotumiwa na watu wengi chuoni hapo.
“Napenda kuwafahamisha kuwa kamera za CCTV tulizonazo zimefungwa katika vyumba vya madarasa kulingana na teknolojia iliyopo sasa na ni jambo la kawaida na zimefungwa kwa lengo la kuimarisha ulinzi kwa lengo la kutoa wataalam waliobobea na si kama ilivyoandikwa kwa kupotoshwa na gazeti hilo na baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa zinalenga kudhibiti vitendo vya ngono darasani” amesema Prof. Mjema.
Aidha kuhusu hali ya ulinzi na usalama chuoni hapo amesema kuwa chuo hicho kimekuwa na utaratibu wa kuweka walinzi getini kwa miaka 49 na kuongeza kuwa hakuna walinzi wapya walioajiriwa kwa ajili ya kukagua mavazi ya wanafunzi  hao  huku akibainisha kuwa utaratibu uliopo sasa wa kukagua vitambulisho kwa wanafunzi wanaoingia chuoni hapo na wageni wengine wanaoingiia ni wa kawaida kwa ajili ya usalama wa chuo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa chuo hicho amesema kuwa chuo hicho kitaanza kutoa masomo ya juu kwa ngazi ya shahada za uzamili  kuanzia mwaka ujao wa kitaaluma na kutoa wito kwa wananchi kuichangamkia fursa hiyo.
Pia amesema kuwa chuo hicho kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha “Eastern Finland” kitaanza kutoa shahada za umahiri na kufafanua kuwa wataalam wa kuifanya kazi hiyo hapa nchini wapo.
“Tutaanza kutoa mafunzo kwa ngazi ya shahada za uzamili katika mwaka ujao wa kitaaluma, wahadhiri wanaofundisha sasa hapa chuoni wana elimu za juu hivyo kuwezesha mchakato huo kuanza”
Katika kuboresha kiwango cha elimu chuoni hapo Prof. Mjema ameeleza kuwa Chuo chake  tayari kimeingia mkataba na chuo Kikuu cha masuala ya Teknolojia cha Shenyang , kilichopo nchini china ambapo wanafunzi wa vyuo vya CBE nchini wataweza kwenda China kumalizia masomo yao kwa mfumo wa kubadilishana.
“ Ni hatua nzuri katika maboresho ya elimu katika chuo chetu kwa kushirikiana na vyuo vya nje hasa Finland na China na sasa baadhi ya wanafunzi wameshaanza kunufaika” ameeleza Prof. Mjema.

No comments: