Social Icons

Sunday 24 November 2013

CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM CHAMTUNUKU NGUGI WA THIONG'O UDAKTARI WA FASIHI



Ngugi+ClipKaimu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Nicholaus Kuhanga (Kushoto) akimtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari Mtunzi wa Vitabu vya Kiafrika, Profesa Ngugi wa Thiong’o kwenye Mahafali ya 43 ya chuo hicho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam jana. PICHA | VENANCE NESTORY 
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimemtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi ya Lugha, Profesa Ngugi wa Thiong’o kutokana na mchango wake mkubwa kwa Bara la Afrika katika kujikomboa kiakili dhidi ya ubeberu wa lugha za kigeni.
Ngugi ambaye ni nguli wa fasihi za lugha na pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha California huko Marekani, alitunukiwa shahada hiyo jana, Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya 43 ya UDSM.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema chuo kimeamua kumpa shahada hiyo kutokana na mchango wake wa kupinga chuki na dharau zinazofanywa na mataifa ya Ulaya dhidi ya lugha za Afrika.
“Katika jitihada hizo, Chuo Kikuu kimeruhusu tasnifu (Thesis) za Shahada ya Uzamili na Uzamivu katika Kiswahili ziwasilishwe katika Lugha ya Kiswahili. Pia Chuo kinasisitiza kuwa tasnifu zote hapa chuoni ziwe na muhtasari mfupi ulioandikwa kwa Kiswahili,” alisema.
Akishukuru baada ya kukabidhiwa shahada hiyo , Ngugi alisema hiyo ni shahada yake ya nane kutunukiwa na vyuo mbalimbali duniani na ya pili kwa  Afrika.   
CHANZO: MWANANCHI



No comments: