Social Icons

Friday, 21 October 2011

Maadhimisho miaka 50 UDSM yanoga

Maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), jana yalifikia kilele huku mafanikio yake yakielezwa na watu waliotoa mchango wao wakitunukiwa tuzo.
Aidha, watu mbalimbali, wakiwemo viongozi mashuhuri na wastaafu waliosoma katika chuo hicho walihudhuria maadhimisho hayo.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika ukumbi wa Nkrumah chuoni hapo na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali mashuhuri.
Mgeni rasmi katika kilele hicho alikuwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alikuwa mgeni maalum.
Wageni wengine mashuhuri waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Asha-Rose Migiro. Wengine ni mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa, Jaji Joseph Warioba, mawaziri na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Baadhi ya viongozi mashuhuri waliotajwa kusoma chuoni hapo ni pamoja na Rais Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Rais Museveni, Dk. Migiro na Lowassa.
Rais Kikwete aliingia ukumbini hapo na Rais Museveni majira ya saa sita mchana na kuelekea katika ukumbi wa Nkrumah ambako watu mbalimbali, wakiwemo wanafunzi walifurika kushuhudia.
WANAFUNZI WAELEZA MATATIZO YAO
Wakati Rais Kikwete na Rais Museveni wakielekea katika ukumbi huo, njiani walipokewa na mabango ya wanafunzi wa chuo hicho waliokuwa wakilalamikia kutopata mikopo na mazingira magumu ya kusomea.
Wanafunzi hao walianza kujipanga mistari kuelekea kwenye ukumbi ilikofanyika sherehe hiyo kuanzia majira ya saa mbili asubuhi kama ratiba ilivyokuwa inaonyesha huku wakiwa na mabango yao ambapo wakati huo mengi walikuwa wameyakunja.
Wanafunzi hao walianza kuimba na kunyanyua mabango yao mara baada ya Rais Kikwete na mgeni wake kuanza msafara wa kuelekea ukumbi wa Nkrumah.
Walikuwa wakiimbia kwa sauti kubwa “msiilipe Dowans, msiilipe Dowans, kama sio juhudi zako Nyerere mafisadi wangesoma wapi, tunalala nje, tunalala nje, hatuna mikopo hatuna mikopo.”
Baadhi ya wahadhiri akiwemo Mhadhiri maarufu wa chuo hicho, Bashiru Ally, walionekana wakiwasihi wanafunzi hao na wakijaribu kuwatulinza na hatimaye walitulia baada ya kujadiliana nao kwa muda mrefu.
Baadhi ya mabango ya wanafunzi hao yalisomeka, mtoto wa mkulima hapati mkopo, mmesoma bure, lecture Nkrumah malazi Bagamoyo je, ni haki? Tunalala nje wakati mafisadi wanatesa.
KIKWETE AAHIDI MIKOPO ZAIDI
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Rais Kikwete alisema serikali yake inaweka mikakati kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wanaojiunga na vyuo vikuu binafsi wanapata mikopo na kuboresha mfumo wa utoaji wa mikopo.
Alisema kwa kuwajumuisha wanafunzi wa vyuo binafsi katika mikopo, bajeti ya mikopo ya elimu ya juu imepanda kutoka Sh. bilioni 56.1 mwaka 2005/6 hadi kufikia Sh. bilioni 317.9 mwaka huu.
Alisema hali hiyo imeiwezesha serikali kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo ya elimu ya juu kutoka wanafunzi 16,345 mwaka 2005/6 hadi kufikia wanafunzi 93,105 mwaka huu.
“Idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza 24,625 watakaopata mkopo mwaka huu ni kubwa kulinganisha na idadi ya wanafunzi kama hao wa vyuo vikuu waliopata mikopo mwaka 2005, tutaendelea kuboresha mfumo wa utoaji wa mikopo uwe rahisi zaidi na wa wazi lengo likiwa ni kumaliza malalamiko ya wanafunzi ambao hawaridhishwi na mfumo wa sasa,” alisema.
Kikwete alisema serikali pia itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kujenga vyuo vikuu nchini.
MUSEVENI AIMWAGIA SIFA UDSM
Kwa upande wake, Rais Museveni, alisema UDSM imetoa mchango mkubwa si tu kwa wasomi wa Tanzania bali kwa wananchi wengi wa Afrika nzima.
“Nimekuja hapa kuwapongeza Watanzania, hongereni sana na kipekee nampongeza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa uamuzi wake wa kuanzisha chuo hiki ambacho mafanikio makubwa mmeyapata,” alisema Rais Museveni.
Alisema mwanasheria wa kwanza wa Uganda alisoma katika chuo hicho na Jaji Mkuu wa nchi hiyo alisoma hapo pia. Alimtaja pia Makamu wa rais wa Sudan kuwa alisoma katika chuo hicho.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema chuo hicho kimekuwa kikipata mafanikio kila mwaka na kimekuwa moja ya vyuo vinavyoheshimika sana barani Afrika na duniani.
Profea Mukandala alisema chuo hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961, kimekuwa kikitoa wataalamu wa fani mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika ustawi wa taifa.
Profesa Mukandala alifafanua kuwa kila mwaka chuo hicho kinatoa wahitimu 6,000.
WALIOTOA MCHANGO WATUNUKIWA
Watu waliotoa mchango mkubwa katika kuanzishwa kwa UDSM ambao wakitunukiwa tuzo maalum jana ni pamoja na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere; Profesa Robert Cranford Pratt, Dk. Wilbard Kumalija Chagula; Chifu Patrick Kunambi; Profesa Arthur Brian Weston na Jaji Julie Catherine Manning kwa kuwa mwanamke wa kwanza kusoma katika chuo hicho.
CHANZO: NIPASHE

No comments: