TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Jumatatu ijayo itatoa utaratibu wa kuomba udahili kwa vyuo vya elimu ya juu vyenye nafasi za ziada kwa mwaka wa masomo 2011/12, hivyo wanafunzi wasio na udahili na vyuo vyenye nafasi wasubiri wakati huo. Hata hivyo, wakati TCU ikitoa taarifa hiyo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imesema udahili huo hauhusiki na mikopo kwa kuwa tayari wamekamilisha hatua ya wanaopata mkopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na bajeti iliyotengwa kwa mwaka huu imekwisha. Katika taarifa yao kwa umma waliyoitoa, TCU ilisema hivi sasa utaratibu huo unaandaliwa, hivyo vyuo vya elimu ya juu vinapaswa kutuma taarifa zao mapema ili programu husika ziweze kuongezwa kwenye mfumo kabla ya Septemba 26, mwaka huu. Aidha, TCU imesema kutokana na hatua hiyo ni vyema vyuo vikasubiri kutoa matangazo ya udahili ili kuondoa mkanganyiko unaojitokeza kwa wanaotaka kuomba kusoma hadi hapo watakapotoa utaratibu huo na kuvitaka kwa sasa vyuo kutuma taarifa TCU kama vina nafasi. Hatua hiyo inatokana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kutoa matangazo ya udahili wiki iliyopita, ikiwa ni awamu nyingine ili kutoa fursa kwa waliokosa udahili na wenye uwezo wa kujilipia, kuomba tena kutokana na chuo hicho kuwa na nafasi kwa baadhi ya programu. Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Taaluma, Profesa Makenya Maboko akizungumza na gazeti hili kuhusu taarifa hiyo, alisema chuo hicho hakikuwa na taarifa ya TCU kuhusu utaratibu huo wa kutakiwa kusubiri hadi Septemba 26, ndipo watangaze. Profesa Maboko alisema kutoa matangazo hayo hakukuwa na maana ya kutoishirikisha TCU kwa kuwa hakuna udahili ungeweza kufanyika nje ya Tume hiyo na watapeleka taarifa kama walivyoelekezwa kuhusu programu zenye nafasi katika chuo chao. Akifafanua kuhusu hilo jana, Ofisa Habari wa TCU, Edward Mkaku alisema utaratibu huo unafahamika na vyuo vyote na ni awamu ya tatu baada ya awamu ya kwanza kufanyika Mei, ya pili Agosti na ya tatu Septemba na kuongeza kuwa hata hao wanaoomba Bodi na kukosa mikopo, husoma kama wanafunzi binafsi hivyo ni vizuri kusubiri utaratibu huo. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa aliliambia gazeti hili kuwa, udahili huo hauihusu bodi hiyo kwa kuwa ilishafunga utoaji wa mikopo kwa bajeti ya mwaka huu wa masomo (2011/12). Hivi karibuni, HESLB ilitoa tangazo la majina ya wanafunzi waliopata mikopo na ya waliokosa.
Chanzo - Habari Leo
No comments:
Post a Comment