Jeshi
la polisi mkoani Morogoro linamsaka mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Mwita Marwa (30) kwa tuhuma za
kumuua kwa kumnyonga mpenzi wake Kibua Adam (39) baada ya kutokea
kutokuelewana kati yao.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema tukio hilo lilitokea
Januari 22 mwaka huu katika eneo la Modeco Manispaa ya Morogoro ambapo
mwanafunzi huyo alitoweka baada ya tukio hilo.
Amesema
siku ya tukio mwanafunzi huyo na mpenzi wake ambaye ni mhudumu wa baa
walichukua chumba katika nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kama Aluta
ambapo walilala lakini baadaye mwili wa marehemu ulikutwa chumbani.
“Dada
huyu mkazi wa Kihonda alikutwa ameachwa chumbani akiwa ameshafariki na
baada ya uchunguzi ilionekana kwamba marehemu alinyongwa shingo kabla ya
kifo chake,” amesema Kamanda Matei.
Hata
hivyo, kamanda huyo amesema baada ya tukio hilo mtuhumiwa alimwandikia
ujumbe wa simu dada wa marehemu aitwaye Happiness Adamu ujumbe akisema
kwamba tayari marehemu keshatangulia na yeye mtuhumiwa atafuata.
“Nasikitika
sana hamtatuona hapa duniani Mwita na Kibua, mimi ninayeandika meseji
hii ni Mwita, nikimaliza nakunywa sumu au vidonge nife na mimi nimechoka
na dunia na Kibua yeye keshatangulia, njooni hapa Aluta Bar mtutoe
chumbani tulipolala,” ulisomeka ujumbe huo.
Hata
hivyo, watu wa karibu wa marehemu ambao hawakutaka kutaja majina yao
walisema marehemu alikuwa na mpenzi mwingine kabla ya Mwita na
walipokorofishana ndipo alipoamua kuwa na Mwita lakini siku chache kabla
ya tukio alimwambia Mwita kwamba mpenzi wake wa awali amejirekebisha
hivyo anataka kurejeana naye jambo ambalo mtuhumiwa alikuwa analipinga.
Kamanda
Matei amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa
ya Morogoro na jeshi hilo bado linaendelea na jitihada za kumsaka
mtuhumiwa.
No comments:
Post a Comment