Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda akisalimiana na viongozi
na wafanyakazi wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam
alipowasili chuoni hapo kuzindua Bodi mpya ya uongozi ya Chuo hicho leo.
Na Aron Msigwa –MAELEZO
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda amezindua rasmi Bodi ya
Uongozi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na kuitaka bodi hiyo kufanya
kazi zake kwa kuzingatia sheria na kushirikiana na menejimenti ya chuo
hicho kuweka mikakati na mipango ya maendeleo itakayokiwezesha chuo
hicho kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza
na viongozi na wajumbe wa bodi hiyo leo jijini Dar es salaam, Dkt.
Kigoda amesema serikali inayo imani kubwa na Mwenyekiti na wajumbe wa
Bodi hiyo walioteuliwa na kwamba watatimiza majukumu yao kikamilifu na
kukiwezesha chuo hicho kufikia malengo na matarajio ya watanzania ya
kuendelea kuzalisha wataalam bora wa fani za biashara.
“Ninaamini
kuwa Bodi niliyoizindua leo itasimamia shughuli za chuo hiki kwa
kufuata misingi ya uadilifu,utawala bora na kuongeza chachu ya kuleta
huduma bora kwa wananchuo na umma” Amesisitiza Dkt. Kigoda.
Amesema
viongozi na wajumbe wa Bodi walioteuliwa wanalojukumu la kusimamia
ustawi wa chuo hicho wakiwa chombo cha juu cha utoaji wa maamuzi na
usimamizi wa masuala mbalimbali ya chuo hicho ikiwemo uidhinishaji wa
matumizi ya chuo yanayoendana na mapato ya chuo, uteuzi wa Mkuu wa Chuo
na watumishi wengine na uidhinishaji wa viwango vya ada.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda akizungumza na wajumbe wa
Bodi ya Chuo cha CBE na menejimenti ya chuo hicho kabla ya kuzindua
rasmi Bodi mpya ya uongozi ya chuo hicho leo.
Akizungumzia
mabadiliko ya chuo hicho toka kuanzishwa kwake mwaka 1965 Dkt. Kigoda
amesema yamehusisha mabadiliko makubwa ya mitaala ya kufundishia ili
kuwafanya wanafunzi na wahitimu waweze kupanua ufahamu wao kwa kuwa na
uwezo wa kukabiliana na ushindani wa soko la ajira kwa kuongeza fursa
za ajira katika sekta ya umma na binafsi pamoja kuwajengea uwezo
wahitimu waweze kujiajiri wenyewe.
Kwa
upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema akizungumza wakati
wa kuwakaribisha wajumbe walioteuliwa chuo hapo amesema kuwa wao kama
viongozi wa chuo hicho wataendelea kusimamia msingi wa kuanzishwa kwa
chuo wa kuendelea kuzalisha wataalam bora katika nyanja za biashara na
sekta ya uendeshaji viwanda nchini.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda (kulia) akimkabidhi
mwongozo wa utendaji kazi Mwenyekiti wa Bodi iliyoteuliwa ya uongozi wa
Chuo cha Elimu ya Biashara, Prof. Mathew Luhanga (kushoto) leo jijini
Dar es salaam.
Amesema
kuwa wao kama menejimenti ya chuo hicho watashirikiana na uongozi na
wajumbe wa bodi iliyoteuliwa kusimamia rasilimali na miundombinu ya chuo
hicho ili kiendelee kutoa huduma bora kwa wanafunzi na wananchi wengi
Zaidi kwa wakati.
Naye
Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi ya Chuo hicho Prof. Eleuther
Mwageni akizungumza kwa niaba ya uongozi na wajumbe wa bodi iliyoteuliwa
amesema kuwa Bodi iliyoteuliwa itatekeleza majukumu yote
yaliyoanishwa kwa mujibu wa sheria.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda (katikati) akizungumza
jambo na viongozi na wajumbe wa Bodi mpya ya uongozi ya Chuo cha Elimu
ya Biashara (CBE) iliyoteuliwa alipokuwa akitembelea maeneo mbalimbali
ya chuo hicho leo jijini Dar es salaam. Kutoka kushoto ni Mkuu wa chuo
hicho Prof. Emanuel Mjema akifuatiwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi Prof.
Eleuther Mwageni na Prof. Mathew Luhanga ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya
Uongozi ya CBE (kulia).
Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Emanuel Mjema (kushoto)
akimwonesha Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda baadhi
ya maeneo ya chuo yaliyokuwa yamevamiwa na watu na kujengwa majengo
yakiwa wazi baada ya kubomolewa kufuatia uongozi wa chuo hicho kuendelea
na juhudi za kuyarudisha maeneo yote yaliyokaliwa kinyume cha sheria
chini ya umiliki wa chuo.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah (katikati)Kigoda akiwa katika
picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Uongozi wa Chuo cha CBE na
Menejimenti ya CBE leo jijini Dar es salaam.(Picha na Aron Msigwa-
MAELEZO).
Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Tumieni mtandao huu ni wenu nyote.
No comments:
Post a Comment