Social Icons

Friday 14 November 2014

WANAFUNZI BORA CBE WAPATA TUZO.



Na. Aron Msigwa – MAELEZO


Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam kimetoa tuzo kwa wanafunzi bora 12 waliohitimu na kufanya vizuri katika masomo yao kwa mwaka wa masomo 2014/2015 ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa chuo hicho kuenzi na kuthamini mchango walioutoa katika maendeleo ya taaluma chuoni hapo.

Akikabidhi tuzo hizo katika hafla fupi iliyofanyika jana jijini Dar es salaam, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mwenyekiti wa sasa wa wanafunzi  waliomaliza chuo cha CBE, Bw. Harry Kitilya amesema kuwa wahitimu hao wanayo nafasi kubwa ya kutumia elimu waliyoipata na kuwa mfano katika kuleta mabadiliko nchini.

Amesema chuo hicho tangu kuanzishwa kwake  mwaka 1965 kimekua mfano wa kuigwa kwa kuwajengea uwezo wanafunzi wanaohitimu  ili waweze kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Biashara nchini kwa kuongeza  nafasi za ajira kwa kujiajiri wenyewe  kupitia shughuli za ujasiriamali,uanzishaji wa makapuni na miradi mbalimbali.

Bw.Kitilya amewataka wahitimu hao kujiendeleza zaidi kielimu ili waweze kukabiliana na ushindani wa ajira uliopo hususan katika soko la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii na kuepuka vitendo vya rushwa na uzembe pindi wanapoingia katika ajira.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema akizungumza na wahitimu wa mwaka 2014 wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo ulioshuhudiwa na wanafunzi waliosoma miaka ya nyuma ni utaratibu wa chuo hicho kuenzi na kuthamini juhudi walizozionyesha katika taaluma.

 Amesema utoaji wa tuzo hizo umehusisha  fani za Uhasibu,Udhibiti wa Biashara, Usimamizi wa Masoko,Manunuzi na Ugavi na kuongeza kuwa utafanyika katika kampasi nyingine za chuo hicho zilizoko Zanzibar, Mbeya, Dodoma na Mwanza.

“Siku ya leo mbali na zoezi hili la utoaji wa tuzo, wahitimu wote wa sasa na wa zamani wanakutana kujadili namna ya uendelezaji wa chuo chetu, siku hii ni muhimu sana kwa kuwa inaongeza ushiriki wao katika kujadili masuala mbalimbali ya kukiendeleza chuo” Amesema Prof. Mjema.

Ameongeza kuwa lengo la kuwakutanisha wahitimua wa miaka iliyopita ni kujenga umoja imara na kupata mrejesho kutokana na huduma wanazozitoa kwa jamii, mahitaji ya soko la ajira na mabadiliko ya kiuchumi yaliyopo.
Kwa upande wao baadhi ya wahitimu wa mwaka 2014 na wale miaka iliyopita wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa hafla hiyo, wameiomba Serikali kendelea kupanua wigo wa Elimu ya Biashara kwa kuongeza matawi mengi zaidi kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi katika maeneo yao.

Wameiomba Serikali kupitia wizara ya Viwanda na Biashara kuwaendeleza na kuwawezesha wahitimu wanaoonyesha nia ya kujiajiri wenyewe na kuanzisha makampuni yao hapa nchini.

Aidha ,wametoa wito kwa walimu kutoa mafunzo yanayoendana na mabadiliko ya kiuchumi yanayotokea duniani ili kuwawezesha kukidhi soko la ajira  huku wakitoa wito  kwa wahitimu wa vyuo kujenga utamaduni wa kujitolea ili waweze kupata uzoefu
Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Tumieni mtandao huu ni wenu nyote.

No comments: