Social Icons

Wednesday 27 June 2012

3000 kukosa udahili vyuo vikuu


Fredy Azzah 
TUME ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), imesema kuwa wanafunzi 3000 kati ya 40,000 waliomba kujiunga na vyuo mbalimbali nchini wamekosa udahili kutokana na kasoro mbalimbali. 

Katibu Mtendaji wa TCU Profesa Sifuni Mchome, aliliambia gazeti hili kuwa wanafunzi 37,000 ndio waliofanya maombi hayo kwa usahihi kupitia mfumo  unaojulikana kama  'Central Admission System', udahili wao una makosa mbalimbali. 

“Jana (juzi) niliangalia na kuona wanafunzi 40,000 ndio wamefanya maombi, hao 3000 ndio wenye makosa mbalimbali, wengine wameingia tu na kufikiri ndiyo wameshafanya maombi na makosa mengine kama hayo,” alisema Profesa Mchome na kuongeza: “Barua pepe ambazo zitakuwa zimewarudia ni vyema wakazifanyia kazi kabla ya siku ya mwisho ambayo ni Juni 30.” 

Alisema kuwa Julai 6 TCU itakutana na vyuo ili kupitia majina ya waombaji ambapo Julai 15 watakaa na kufanya udahili kamili kwa kuwapangia wenye sifa kwenye vyuo walivyoomba. “Nawaambia wanafunzi wasubiri huo udahili wa Julai 15,” alisema Profesa Mchome. 

Katika hatua nyingine, wakuu wa vyuo na wadau wengine wa vyuo vikuu, walikutana jana jijini Dar es Salaam kujadili mfumo wa pamoja wa tuzo (University Qualification Framework). Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kujadili mfumo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Selestine Gesimba, alisema mfumo huo utasaidia kuweka viwango sawa vya mafunzo yanayotolewa na vyuo vikuu vyote nchini.

 Katika hatua nyingine, Profesa Mchome alizungumzia wizi uliotokea katika ofisi hiyo usiku wa kuamkia juzi akisema kuwa, mali zilizopotea ni kompyuta 10 huku thamani yake ikiwa haijajulikana.
Chanzo: Mwananchi

No comments: