Social Icons

Wednesday 7 March 2012

Taarifa za uwepo wa chuo FEKI NCHINI

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania imepokea taarifa kupitia matangazo yanayotolewa na chuo kinachojiita “Japan Bible Institute Graduate School of Theology” kikijitangaza kwamba kinatoa shahada mbalimbali za uzamivu (PhD) kwenye nyanja za dini na jamii. Chuo hiki kinajitangaza kwamba kinawakilisha tawi la taasisi iliyopo nchini Marekani na kwamba makao yake makuu kwa bara la Afrika yapo Dar es Salaam, pamoja na kwamba eneo halisi ofisi zao zilipo haijaelezwa kwenye matangazo yao.

Tume inachukua fursa hii kuuarifu umma kwamba chuo hiki hakitambuliki kwa mujibu wa sheria na kwamba wamiliki wa Japan Bible Institute Graduate School of Theology hawana kibali cha kutoa elimu ya chuo kikuu ambayo inatambuliwa hapa nchini. Tume inatoa tahadhari kwa umma kuepuka ulaghai ambao unafanywa na watu katika eneo hili la elimu ya juu na hivyo umma unashauriwa kuchukua tahadhari kwani vyeti watakavyotolewa havitambuliwi na Tume na hivyo haviwezi kutumika hapa nchini.

Pia, wamiliki wa chuo hiki na wawakilishi wake waliopo Tanzania wanapewa onyo kuacha mara moja kutoa matangazo ya shahada za aina hiyo hapa nchini bila kufuata taratibu. Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaye kwenda kinyume na tangazo hili.

Aidha, Tume inapenda kuwaarifu watu wote wenye lengo la kuanzisha vyuo vikuu nchini au kutoa programu za vyuo vikuu wawasiliane na Tume ili kupata maelekezo juu ya taratibu zinazotakiwa kufuatwa. Pia umma unasahauriwa kutoa taarifa kwa Tume ama vyombo vingine vya dola pale ambapo wana wasiwasi na uhali wa programu ama tuzo inayotangazwa au kutolewa na taasisi yoyote bila kufuata taratibu.

Imetolewa na:
Katibu Mtendaji
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
S.L.P. 6562
DAR ES SALAAM

No comments: